Rutubisheni utu wenu kwa njia ya imani bila ya kuichafua kwa kukumbatia malimwengu!
Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 10 Januari 2014 amekutana, amezungumza na
kuwashukuru wafanyakazi walei wanaotoa huduma ya kutukuka mjini Vatican, katika mapokezi
ya viongozi mbali mbali wanaofika mjini Vatican kumtembelea Khalifa wa Mtakatifu Petro
pamoja na kumsindikiza Baba Mtakatifu wakati wa shughuli zake za kitume kwenye Uwanja
au Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Baba Mtakatifu anasema huduma
yao ni muhimu sana kwa watu mbali mbali wanaofika mjini Vatican ili kukutana na kuzungumza
na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Wao kimsingi ni kioo cha maisha na utume wa Kanisa
mjini Vatican, jambo linalohitaji, uungwana na ukarimu kwa wageni. Maisha ya kiutu
hayana budi kurutubishwa na imani inayotolewa ushuhuda bila kuichafua kwa kutaka kukumbatia
malimwengu.
Baba Mtakatifu anasema, Kanisa linahitimisha Kipindi cha Noeli,
kilichowapatia waamini fursa ya kumtafakari Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, akazaliwa
mjini Bethelehemu, kielelezo cha upendo wa Mungu kwa binadamu. Mwanga ulioletwa kwa
kuzaliwa kwa Yesu Kristo uwe ni sehemu ya ushuhuda wa maisha ya waamini katika uhalisia
wa maisha yao ya kila siku: ndani ya familia na sehemu zao za kazi. Furaha ya imani
ijioneshe kwa namna ya pekee katika upendo, ukarimu pamoja na kuwajali wengine.
Baba
Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa kuwaweka wafanyakazi hao walei pamoja na familia
zao chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria, ili aweze kuwasindikiza na kuwalinda
katika hija ya maisha yao hapa duniani.