Mwaka wa shughuli za Mahakama kuu ya Vatican wafunguliwa rasmi!
Kardinali Raymond Leo Burke, Mwenyekiti wa Mahakama kuu ya Vatican, Jumamosi, tarehe
11 Januari 2014 ameufungua Mwaka wa 85 wa shughuli za Mahakama kuu ya Vatican kwa
Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Kwa
upande wake, Professa Gian Piero Milano, Mhamasishaji wa amani Mahakama kuu ya Vatican
anasema kwamba, wao wanatekeleza shughuli zao kwa kuzingatia utu na heshima ya binadamu.
Wanapania kujenga na kuimarisha upendo, udugu na mshikamano kati ya watu pamoja na
kusimama kidete kulinda na kutetea haki kwa kuzingatia ukweli, upendo, ili kuchangia
ustawi na maendeleo ya wengi mintarafu uwezo na fursa za kila mtu. Yote haya yanalenga
ujenzi wa amani ya kweli kati ya watu.
Hotuba ya ufunguzi kuhusu shughuli za
Mahakama kuu ya Vatican imegusia kwa namna ya pekee kuhusu: vyanzo vya sheria za Mahakama
za Vatican, Marekebisho ya Sheria yaliyofanywa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto
XVI; sheria zinazotekelezwa chini ya uongozi wa Papa Francisko pamoja na baadhi ya
marekebisho ya taratibu na sheria za makosa ya jinai.
Jambo kubwa zaidi ni
sheria za udhibiti wa utakatishaji wa fedha haramu kwa ajili ya kugharimia vitendo
vya kigaidi pamoja na ushirikiano wa vyombo mbali mbali mjini Vatican katika utekelezaji
wa sheria za makosa ya jinai. Amefafanua kwa kina na mapana, shughuli za Mahakama
kuu ya Vatican zilizotekelezwa katika Mwaka wa Mahakama 2012 - 2013.