2014-01-11 14:58:20

Miaka 50 ya Tume ya Ushirikiano wa kitamaduni kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa ya Kiorthodox ni kielelezo cha hija ya upatanisho na udugu!


Imekwisha timia miaka 50 tangu Tume ya ushirikiano wa kitamaduni kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa ya Kiorthodox na Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki. Hizi zilikuwa ni cheche za ushirikiano na majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa hata kabla ya kuhitimishwa kwa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Hii ilikuwa ni hija ya upatanisho na udugu; mambo yaliyopelekea hata Papa Paulo VI akafanikiwa kukutana na kuzungumza na Patriaki Atenagora wa Costantinopoli kwa wakati huo!

Hapa waamini kutoka Makanisa mbali mbali wakaanza mchakato wa kutaka kufahamiana na kushirikiana kwa dhati, hususan majandokasisi waliokuwa wanajiandaa kwa jili ya utume ndani ya Kanisa. Huu ukawa ni mwanzo wa Tume ya Ushirikiano baina ya Makanisa ya Kiorthodox.

Tangu wakati huo hadi sasa imeendelea kutoa nafasi za masomo kwa wanafunzi, makleri na walei kutoka Mashariki wanaotaka kujiendeleza katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki sanjari na kuunga mkono miradi mingine inayojikita katika majadiliano ya kiekumene!

Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na Kamati ya ushirikiano kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa ya Kiorthodox pamoja na Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki, Jumamosi, tarehe 11 Januari 2014 kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 tangu Tume hii ilipoanzishwa. Baba Mtakatifu anawashukuru wadau mbali mbali pamoja na wafadhili kwa jitihada zao zilizofanikisha ushirikiano huu. Anawahimiza kuendelea kuchangia kwa hali na mali katika kufanikisha malengo yaliyoko mbele yao.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha wanafunzi wanaoendelea na masomo yao hapa mjini Roma kwamba, hii ni fursa ya majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa, kwa leo na hapo kesho. Amewahakikishia kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa na Askofu wa Roma.

Ni matumaini yake kuwa wataendelea kujitajirisha katika maisha ya kiroho na kitamaduni, huku wakiendelea kujisikia kuwa ni wageni, lakini zaidi kama ndugu wamoja katika imani kwa Kristo na Kanisa lake.







All the contents on this site are copyrighted ©.