2014-01-11 08:23:19

Huduma makini kwa watu wa Mungu ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya!


Caritas na Uinjilishaji mpya ndiyo kauli mbiu iliyoongoza semina ya thelathini na saba ya Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Cameroon iliyoanza tarehe 6 Januari hadi tarehe 11 januari 2014 mjini Douala, Cameroon. RealAudioMP3
Semina hii ilianza kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mitume Petro na Paulo na kuwashirikisha: Maaskofu, Mapadre, Watawa na Waamini walei kutoka sehemu mbali mbali za Cameroon.
Maadhimisho haya ni muhimu sana katika maisha na utume wa Familia ya Mungu nchini Cameroon, wakati huu Kanisa Barani Afrika linapoendelea kujiwekea mikakati ya Uinjilishaji Mpya kwa njia ya huduma makini zinazotolewa katika sekta mbali mbali za maisha.
Haya ni maneno ya Monsinyo Sebastien Mongo Behon, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Cameroon, ambaye pamoja na mambo mengine amekazia umuhimu wa Kanisa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Hawa ni wagonjwa, maskini, watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, wakimbizi, wahamiaji na wote wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali katika maisha.
Kwa upande wake, Askofu mkuu Samuel Kleda, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Cameroon anasema, Kanisa halina budi kuzivalia njuga kero zinazowakabili waamini na wananchi wa Cameroon katika ujumla wake, kwa kuangalia kwa kina na mapana dhamana na utume wa Caritas Cameroon katika mchakato wa kukabiliana na changamoto hizi. Lengo ni kutaka kuhakikisha kwamba, Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki, Caritas linakuwa ni kichocheo kikuu cha Uinjilishaji Mpya kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Caritas ni kielelezo cha upendo na mshikamano unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake ! Huduma za kijamii na kiuchumi ziwe ni kielelezo cha mchango wa Kanisa katika harakati za kumkomboa mwanadamu: kiroho na kimwili, tayari kumwonjesha Injili ya Furaha. Kanisa halina budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kama alivyofanya Kristo mwenyewe na kama ambavyo Baba Mtakatifu Francisko anavyoendelea kuhimiza katika maisha na utume wa Kanisa.
Naye Bwana Michael Roy, Katibu mkuu wa Shirikisho la Misaada la Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis anasema, Uinjilishaji Mpya ni mchakato unaopania kuliwezesha Kanisa kurithisha Imani ya Kikristo, kama ilivyoelekezwa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu Uinjilishaji, iliyoadhimishwa Mjini Vatican kunako Mwaka 2012.
Huduma ya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni asili ya Kanisa, kwani hakuna Uinjilishaji Mpya pasi na huduma makini, kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji. Imani inayomwilishwa katika huduma ya upendo inaleta mguso mkubwa kwa watu wanaoipokea, kwani huu ni ushuhuda wa upendo wa Mungu kwa ajili ya watu wake pasi na upendeleo. Ni huduma inayowawezesha waamini kuwa ni Wamissionari wa Habari Njema ya Wokovu kwa kujiinjilisha kwanza wao wenyewe!
Mama Kanisa anatambua mchango unaotolewa na wadau mbali mbali katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya, lakini huduma ya upendo na mshikamano wa kidugu ina kishindo kikuu katika maisha ya watu. Haitoshi kufahamu mbinu na mikakati ya Uinjilishaji Mpya, bali jambo la msingi ni kutambua ikiwa kama wadau wenyewe wa Injili ni mashahidi wanaoaminiwa na kuthaminiwa na Jamii inayowazunguka!








All the contents on this site are copyrighted ©.