Askofu Abou Khazen ni mapambazuko ya matumaini huko Mashariki ya Kati, ili kujenga
na kuimarisha haki na amani dhidi ya chuki na vita!
Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya
Mashariki, Jumamosi, tarehe 11 Januari 2014, amemweka wakfu Askofu Georges Abou Khazen
wa Jimbo la Kitume la Aleppo, lililoko nchini Lebanon. Katika mahubiri yake, amekumbusha
umuhimu wa amani ya kweli ambayo kwa sasa ni kilio kikuu cha Jumuiya ya Kimataifa.
Kardinali Sandri amewakumbuka wote wanaoendelea kuteseka nchini Syria kutokana na
vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo inaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na
mali zao.
Kardinali Sandri amewakumbuka na kuwaombea Askofu Boulos Al - Yazigi
wa Kanisa la Kiorthodox la Kigiriki pamoja na Askofu Youhanna Ibrahim wa Kanisa la
Kiorthodox la Syria, ambao walitekwa nyara Aprili, 2013 hadi sasa hawajulikani mahali
waliko. Hili ni giza na uvuli wa mauti unaondelea kutanda katika uso wa dunia.
Ni
matumaini ya Kardinali Sandri kwamba, Jumuiya ya Wakristo huko Mashariki ya Kati,
itafanikiwa siku moja kuona mwanga unaofungua njia za kiutu, ili kupambana fika na
umaskini pamoja na mahangaiko ya watu, kwani Mwenyezi Mungu kamwe hawezi kuwaacha
watu wake, bali anatembea nao hatua kwa hatua.
Kuwekwa wakfu kwa Askofu Abou
Khazen, yawe ni mapambazuko ya matumaini kwa Syria, kipindi cha ujenzi wa misingi
ya haki na amani; dhidi chuki na uhasama, ili watu waonje furaha na utulivu wa ndani,
badala ya kuendelea kuelemewa na majonzi na simanzi mioyoni mwao!
Kardinali
Sandri anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kusali kwa ajili
ya kuombea amani nchini Syria; ili watu waweze kujikita katika mchakato unaopania
kujenga na kuimarisha haki, amani na upatanisho wa kitaifa.
Ibada hii imehudhuriwa
na viongozi mbali mbali wa Kanisa kutoka ndani na nje ya Lebanon. Kardinali Sandri
ametoa baraka na mshikamano wa dhati kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili
ya wananchi wanaoishi huko Mashariki ya Kati. Kardinali Sandri anatarajiwa kuhitimisha
hija yake ya kichungaji nchini Lebanon, Jumatatu, tarehe 13 Januari 2014 kwa kukutana
na kuzungumza na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Beirut kinachomilikiwa na kuongozwa na
Shirika la Anthony wa Meroniti.