2014-01-10 09:01:05

Tamko la OASIS kuhusu madai ya Katiba Mpya nchini Zambia


Zambia inapojiadnaa kuadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu ilipojipatia uhuru wa bendera kutoka kwa Mwingereza ni kipindi muafaka kwa viongozi wa Serikali na wadau mbali mbali kusikiliza kilio cha wananchi wa Zambia wanaotaka Katiba Mpya, inayoandikwa kwa misingi ya kidemokrasia na wala si kwa ajili ya kukidhi matakwa na ujanja wa watu wachache nchini humo.

Hili ni tamko la Shirikisho la Umoja wa Makanisa na vyama vya kiraia linalojulikana kama OASIS, kwa viongozi wa Serikali ya Zambia wanaoonekana kana kwamba, wanataka kukwamisha mchakato wa utungaji wa Katiba Mpya ya Zambia, Sheria Mama ambayo tangu Mwaka 1964 imekwisha fanyiwa marekebisho mara nne. Kwa sasa wananchi wa Zambia wanasema, wamechoshwa na kuona Katiba yenye viraka viraka! Serikali katika awamu mbali mbali imekwamisha mchakato wa kutaka kupata Katiba mpya ili ziendelee kukaa madarakani kwa ajili ya mafao yao binafsi, linasema OASIS.

Wananchi wa Zambia wanataka kuona wanasiasa wanaowajibika kwa ajili ya kutafuta mafao ya wengi na kwamba Katiba Mpya ni haki ya wananchi wa Zambia kwa wakati huu, jambo ambalo kamwe halina tena mjadala. Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Uhuru wa Zambia, kiwe ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani; mwaka wa kujisafisha na kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani.

Shirikisho la OASIS katika tamko lake linawaonya wanasiasa wanaotaka kuchezea hisia za wananchi wa Zambia kwamba, wanaweza kukumbana na hasira kali kutoka kwa wananchi ambao wamechoka kudanganywa kwa maneno matamu, bila vitendo vinavyoashilia utashi wa kisiasa katika kuleta mabadiliko ya dhati nchini Zambia. Ubinafsi unaoambatana na harakati za kuzima kwa makusudi mchakato wa demokrasia ni jambo ambalo kamwe haliwezi kukubalika tena!

OASIS inasema, kwa miaka mingi viongozi wa Serikali wametumia dhamana na madaraka yao vibaya kwa ajili ya kulinda na kudumisha masilahi binafsi kwa kuweka pembeni mafao ya wengi. Miradi mikubwa ya kitaifa imeelekezwa kwa ajili ya masilahi binafsi na kwamba, umefika wakati kwa wananchi wa Zambia kutokubali tena kuongozwa na viongozi wasiokuwa na sifa za uongozi.

Viongozi wa kisiasa watambue kwamba, watu wanataka Katiba Mpya. Ni wajibu wa kila Mzambia kudai haki hii msingi na kamwe wasifumbwe mdomo kwa vistisho. Umma kwa sasa una nguvu ya kuzungumzia kuhusu haki zake msingi kwa uhuru kamili bila kuchoka wala kukata tamaa!

Utawala mbovu, usiozingatia sheria, kanuni na katiba ya nchi umewafanya wananchi wa Zambia kukosa Katiba Mpya ambyo kimsingi ni sheria mama ambayo ingeweza kuweka mambo sawa! Wananchi wanataka Katiba Mpya, haraka iwezekanavyo. OASIS inasema, itayashauri Makanisa kutumia muda kidogo kila Jumapili kwa ajili ya kuzungumzia Katiba Mpya ya Zambia, ili kuharakisha mchakato wa kupata Katiba Mpya.

Wanachama wengine wa OASIS wataendelea kujadili na kupembua kwa kina na mapana umuhimu wa wananchi wa Zambia kuwa na Katiba Mpya. Wanasiasa wanakumbushwa kwamba, Mwaka 2014 ni mwaka wa kujisafisha na wala hakuna ujanja wowote utakaozuia Wananchi wa Zambia kupata Katiba Mpya.







All the contents on this site are copyrighted ©.