2014-01-10 08:10:22

Tafakari ya Neno la Mungu, Sherehe za Ubatizo wa Bwana


Mpendwa mwana wa Mungu, tuko tena pamoja katika ile habari ya furaha ndiyo kushirikishana mapendo ya Mungu kwa njia ya meza ya Neno lake. RealAudioMP3

Leo ndipo tunahitimisha kipindi cha Noeli kwa Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana na tunaanza kipindi cha kawaida cha mwaka wa Kanisa. Kumbe leo pia ni Dominika ya kwanza ya kipindi cha kawaida cha mwaka wa Kanisa.

Katika somo la kwanza Nabii Isaya anatupeni habari juu ya mtumishi wa Mungu ambaye anapokea Roho wa Mungu na kazi yake itakuwa kuwahukumu mataifa kwa haki. Ni nuru na mwanga kwa mataifa. Sifa yake nyingine ni mtulivu na mnyenyekevu na hakati tamaa kwa maana mkono wa Mungu uko juu yake. Mtumishi huyu anakabidhiwa Roho wa Mungu kwa sababu ya kazi ya Kimungu ambayo ni kujenga amani na kuunganisha vilivyovunjika.

Kadiri ya Injili ya Luka 4: 18-19 mtumishi huyu ni Yesu Kristo Masiha aliye Mwana wa Mungu. Anakuja kwa ajili ya kutangaza mwaka wa Bwana ambapo wafungwa na vipofu wataondolewa katika shida zao. Kristo amekwisha fika kwetu, kazi yetu sasa ni kupokea ujumbe wake. Namna ya kupokea ujumbe ni kuitika kwanza ule mpango wa Yohane Mbatizaji na Isaya wa kutengeneza njia ya Bwana, kuondoa visiki na mabonde. Ndiyo kusema, tunapaswa kufanya hivyo kwa sababu tunasikia kuwa huyu ajaye hatumii nguvu bali upendo na hivi anahitaji ushirikiano. Kwa jinsi hiyo ni kuweka ubatizo wetu katika matendo kwa makusudi mazima kabisa.

Mtume Petro akielewa vema nia na mpango wa Mungu anasimama kama tusomavyo katika kitabu cha Matendo ya Mitume na kusema, hakika Mungu hana upendeleo, cha msingi ni kufanya bidii ya kumcha Bwana. Oneni jinsi ambavyo Neno la Mungu linavyopiga kasi, anasema Mtume Petro, si tu kwa Wayahudi bali kwa ajili ya watu wote. Hata hivyo kwa nini fundisho hili?, Ni kwa sababu kulikuwa na upinzani dhidi ya ubatizo wa wapagani. Kumbe, Mtume Petro anasema, Kristo mpakwa mafuta wa Bwana amepiga kazi ya kichungaji baada ya kutiwa mafuta na Roho wa Bwana bila kubagua. Ni fundisho kwetu kujiimarisha katika utume na kuimarisha umoja kamili na watu wote milki ya Mungu. Toeni bure kwa maana mmepewa bure.
Mpendwa mwana wa Mungu, daima tangu mwanzo wa Kanisa mpaka leo kumekuwepo maswali juu ya kwa nini Yesu alibatizwa! Sisi waamini wakristu tunao wajibu wa kujibu maswali haya kwa upole na unyenyekevu kwa wale wanaotuuliza tukitumainia daima msaada wake katika kutoa majibu hayo. Ili kuweza kujibu vema maswali hayo yatupasa kutambua yakuwa, kuna tofauti kati ya ubatizo alioutoa Yohane Mbatizaji na ubatizo wa Kikristo.

Ubatizo wa Yohane unaitwa ubatizo wa toba, ambao ulikuwa ukifanyika hata katika vijidhehebu vingine. Ni kwamba watu walikuwa wakizamishwa katika maji na maana yake mmoja aliacha maisha ya zamani ambayo yalichukuliwa na mkondo wa maji! Ilikuwa ndiyo njia ya kuwaingiza katika kundi lake Yohane na tena ilikuwa kwa hiari katika mantiki ya kutaka kujiandaa kwa ajili ya kumpokea Masiha. Hitaji muhimu ili mmoja aweze kubatizwa ilikuwa ni lazima akubali kukiri hali yake ya dhambi. Kwa mantiki hiyo ndiyo maana Mafarisayo na Masadukayo walikataa kubatizwa na Yohane Mt. 11:27-33.

Mpendwa, kama hivi ndivyo basi lazima mmoja aulize swali kwa nini Masiha aombe kubatizwa? Je, jambo hili si kumfanya Bwana awe chini ya Yohane Mbatizaji? Kwa hakika Masiha hakuwa na haja ya kukiri dhambi kwa sababu hakuwa nazo na pia hakuwa na haja ya kubadilisha maisha yake maana Kristu ni yuleyule jana leo na daima! Kutanzua fumbo hilo yafaa kuangalia vema Injili ya Matayo 3: 13-15. Katika sehemu hii tunakutana na majadiliano kati ya Bwana na Yohane Mbatizaji. Yohane anakataa kwanza kumbatiza Masiha akisema wewe unakuja kwangu? Mimi hasa ndiye ninayehitaji kubatizwa nawe na Masiha anasisitiza abatizwe na Yohane akisema acha iwe hivyo kwa sasa maana ndivyo inavyofaa tuyatekeleze yale yote Mungu anayotaka. Hapo Yohane akakubali.

Basi mpendwa msikilizaji, Bwana anatambua kuwa hahitaji ubatizo lakini anataka mwanzoni mwa maisha yake ya hadharani, yaani maisha ya kichungaji awe upande wa wenye dhambi kama alivyoshiriki mwili wa mtumwa na akashiriki taabu za ukimbizi akiwa mtoto mdogo huko Misri. Anataka akae nao na kusafiri pamoja nao wakielekea kileleni, ndio uhuru ambao aliutangaza katika Injili ya Lk 4:18. Toka tendo hilo takatifu na la kicho. Je, wewe mpendwa msikilizaji wajifunza nini? Mimi pamoja nawe nataka kugeuza maisha yangu katika jumuiya yawe ni maisha ya kukaa na wadhambi pasipo kutenda dhambi ili polepole waonje upendo na kubadilika. Ndiyo kusema hukumu na malumbano yasiyo haki dhidi ya wadhambi havifai kadiri ya fundisho la Bwana. Ninyi wachungaji yafaa kuwasaidia wenye shida mbalimbali katika parokia ili wafikie kilele cha uhuru wa wana wa Mungu.

Mpendwa msikilizaji, tukisoma katika Injili ya Mtakatifu Marko 1:7-11tunapata fundisho la unyenyekevu wa Yohane Mbatizaji na unyenyekevu wa Kristo. Yohane Mbatizaji anakiri udogo wake ambao ni wa chini kabisa. Maana hata kushindwa kushika gidamu ya viatu vya Yesu Kristo. Anatufundisha moja kwa moja kuwa safari ya kumpenda Mungu yatudai kushuka mpaka sakafuni. Mkombozi mwenyewe ndiye pia kielelezo hasa cha hali ya juu kuhusu unyenyekevu. Anajishusha kwanza na anakuwa mtu, kana kwamba hiyo haitoshi anaamua kubatizwa wakati hana doa la dhambi. Anatufundisha kujishusha kukaa pamoja na wadhambi, maana tunabatizwa ili kuokolewa katika uvuli wa dhambi ya asili kwanza na kuweza kupokea neema za Mungu.

Bwana anapobatizwa yafaa tuangalie mambo yaliyotokea. Jambo la kwanza ni kupasuka kwa mbingu, ambalo linatupa habari ileile ya Nabii Isaya katika Dominika za majilio. Nabii anauliza mbona umetufanya tukose kukutii? Mbona umetuacha hata tukasahau kukucha wewe Bwana? Is. 63:15-19. Isaya anauliza haya maswali kwa maana ni kama hakuna upatano kati ya mbingu na nchi. Sasa tendo la kupasuka kwa mbingu ni ishara ya mapatano kati ya mbingu na nchi na mpatanishi ni Kristu katika uwezo wa Utatu Mtakatifu.

Jambo la pili ni alama ya njiwa, yatukumbusha kile kilichotokea wakati wa mafuriko ya Noa. Wakati huo mbingu na dunia vilifungwa na njiwa alipotokea akiwa na tawi la mzeituni ilimaanisha kuwa amani imerejeshwa. Ndiyo kusema kwa ishara ya njiwa kuna amani, ni Roho Mtakatifu afanyaye kazi katika Yesu Kristu chanzo cha amani. Pili njiwa katika Agano la Kale alimaanisha nguvu waliyopewa manabii, kwa alama hiyo tunapata kutambua kwa wazi kabisa kuwa Kristu ana nguvu ya kutenda kazi ya Mungu. Sauti kutoka juu yamaanisha kuwa Kristu ni wa juu na pia Mungu anaongea na watu wake kwa njia ya Mwanae mpenzi.

Tukumbuke pia jambo jingine nalo ni lile la Joshua anapowavusha wana wa Israeli pale Jordani, anapovuka mto anapokea roho wa Mungu ili apate nguvu ya kuwafikisha salama katika nchi ya ahadi. Ni katika mantiki hiyohiyo Masiha anapotoka majini Roho wa Mungu anashuka juu yake ili awaongoze wana wa Mungu katika uhuru na kweli ili wafike mbinguni. Watu wanaoongozwa na Bwana kuelekea kwenye uhuru na kweli ndo sisi, wajibu wetu ni kusikia sauti ya huyo mchungaji mwema. (Yn. 10).

Mpendwa, ninakutakieni heri na baraka tele katika sikukuu ya Ubatizo wa Bwana na nakuomba usisahau wajibu wako ulioupokea kwa njia ya ubatizo, na kwa namna hiyo utakuwa unasherehekea pia ubatizo wako kila siku ya maisha yako. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.