2014-01-10 08:26:28

Jumuiya ya Kimataifa haiwezi kufumbia macho maafa yanayoendelea kutoa nchini Syria


Baraza la Kipapa la Sayansi Jamii, limeandaa warsha ya siku moja, kwa ajili ya Syria itakayofanyika hapo tarehe 13 Januari 2014 mjini Vatican kwa kuwashirikisha viongozi mbali mbali kutoka ndani na nje ya Vatican. RealAudioMP3

Warsha hii itagusia hali halisi ilivyo nchini Syria kwa sasa; juhudi za Jumuiya ya Kimataifa katika kutafuta suluhu ya amani nchini Syria pamoja na vikwazo vinavyoendelea kukwamisha azma hii.

Nafasi ya Syria huko Mashariki ya Kati; msimamo wa Serikali ya Marekani, Russia na Umoja wa Mataifa kuhusu vita inayoendelea nchini Syria. Warsha hii itaangalia pia mchango wa dini mbali mbali katika kukuza na kuendeleza amani, upendo na mshikamano huko Mashariki ya Kati. Wajumbe watapata nafasi ya kujadiliana na kushirikishana mang’amuzi yao kuhusu hali ya vita na matumaini ya Jumuiya ya Kimataifa huko Syria.

Baraza la Kipapa la Sayansi jamii linasema kwamba, Jumuiya ya Kimataifa haiwezi kukaa kimya na kufumbia macho maafa makubwa yanayoendelea kujitokeza nchini Syria. Hadi sasa kuna zaidi ya watu 126, 000 ambao wamefariki dunia; kuna watoto yatima zaidi ya 300, 000 tangu vita ya wenyewe kwa wenyewe ilipoanza nchini Syria.

Baba Mtakatifu Francisko ameguswa kwa namna ya pekee na mateso pamoja na mahangaiko ya wananchi wa Syria wanaoendelea kupoteza maisha yao kwa kusema kwamba, viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanawajibika kimaadili kutoa msaada wa hali na mali kwa waathirika wa vita hii sanjari na kukomesha vita ambayo inaendelea kusababisha vifo vya watu wasiokuwa na hatia.

Baba Mtakatifu Francisko pia aliitisha sala na mfungo kwa ajili ya kuombea amani nchini Syria, akiwaalika viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa na Serikali kufanya tafakari ya kina kuhusu dhana ya amani. Ni matumaini ya Vatican kwamba, wadau wakuu katika vita inayoendelea huko Syria watasitisha vita na kuanza mchakato wa majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi; haki na amani.

Umefika wakati wa kusitisha madhulumu na nyanyaso za kidini dhidi ya Wakristo huko Mashariki ya Kati kwa kukazia majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa. Ili kuwa na amani ya kudumu, kuna haja ya kuanzisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa, itakayosimamia uchaguzi mkuu, sanjari na kudhibiti Vikosi vya ulinzi na usalama. Ni matumaini ya Jumuiya ya Kimataifa kwamba, jitihada za makusudi kabisa zitafanyika dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo!








All the contents on this site are copyrighted ©.