2014-01-10 10:49:30

Juhudi za kidiplomasia katika kutafuta suluhu ya migogoro ya kivita Eneo la Maziwa Makuu


Viongozi wakuu wa nchi kutoka Eneo la Maziwa Makuu,Ijumaa tarehe 10 Januari 2014 wameanza mkutano unaopania kutafuta chanzo cha migogoro na kinzani zinazoendelea kufuka moshi na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Lengo la mkutano huu ni kuibua mbinu mkakati utakaowawezesha wananchi kujikita katika mchakato wa kujiletea maendeleo endelevu na kuachana na falsafa ya vita na kinzani ambayo kwa sasa imepitwa na wakati na watu wamechoka kuishi katika hali ya wasi wasi na kukata tamaa ya maisha!

Nchi zinazoshiriki katika mkutano ambao umefunguliwa mjini Luanda, Angola ni pamoja na: Burundi, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, DRC, Kenya, Uganda, Rwanda, Tanzania, Zambia, Sudan Kongwe na Sudan ya Kusini. Nusu ya nchi zinazoshiriki katika mkutano huu zinakabiliana na vita pamoja na kinzani za ndani kwa ndani. Vita inayoendelea kufyeka maisha ya watu Mashariki wa DRC ni kati ya vita ya muda mrefu Barani Afrika. Inakadiriwa kwamba, zaidi ya watu millini tatu wamekwishafariki dunia kutokana na vita huko DRC.

Hii ni vita inayochochewa na watu kutoka ndani na nje ya DRC, wakati mwingine na nchi jirani. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, DRC ni kati ya nchi zilizobahatika kuwa na utajiri mkubwa wa madini yanayotafutwa katika maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa wakati huu. Wachunguzi wa mambo wanasema, utajiri mkubwa wa madini huko DRC imepelekea laana ya vita isiyokoma hata kidogo!







All the contents on this site are copyrighted ©.