Balozi wa Vatican nchini Gambia awasilisha hati za utambulisho
Askofu mkuu Miroslaw Adamczyk, Balozi wa Vatican nchini Gambia, hivi karibuni aliwasili
nchini Gambia tayari kuanza utume wake. Amepokelewa kwa mikono miwili na viongozi
wa Kanisa na Serikali.
Tarehe 5 Novemba, 2013 Askofu mkuu Adamczyk alikutana
na Waziri wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa Kimataifa nchini Gambia Dr. Aboubakar
A. Senghore na baadaye kuwasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais Alhaj Dr. Yahaya
A. J. J. Jameh.
Rais amelipongeza Kanisa Katoliki nchini Gambia kutokana na
mchango wake wa hali na mali katika maendeleo na ustawi wa wananchi wa Gambia, hususan
katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu. Anasema kuna idadi kubwa ya wananchi
wa Gambia ambao wamepata elimu yao kutoka katika shule na taasisi zinazomilikiwa na
kuendeshwa na Kanisa Katoliki, bila ubaguzi wowote wa kidini.
Rais Jameh,
ameelezea kurishwa kwake na uhuru wa kidini nchini Gambia na kwamba, haya ni kati
ya mambo Serikali yake inayapatia kipaimbele cha kwanza, kama sehemu ya mchakato wa
kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na utulivu, chachu makini katika
harakati za wananchi kujiletea maendeleo yao wenyewe!
Rais Jameh amemwomba
Askofu mkuu Miroslaw Adamczyk, kumfikishia salam zake binafsi na zile za wananchi
wa Gambia, heri na matashi mema kwa Noeli na Mwaka Mpya 2014 Baba Mtakatifu Francisko.
Askofu
mkuu Adamczyk amewashukuru wote na kuwapatia kheri na baraka kutoka kwa Baba Mtakatifu
Francisko na kwamba, anawakumbuka katika sala na sadaka yake. Kanisa linawapongeza
wananchi wa Gambia kwa kukuza na kudumisha misingi ya amani, utulivu na kuvumiliana.
Tarehe 3 Novemba 2013, Askofu mkuu Adamczyk aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu
kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Theresa na kutambulishwa kwa Familia ya Mungu nchini
Gambia, kazi iliyofanywa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Banjul. Baadaye, Askofu mkuu
Adamczyk alipata fursa ya kutembelea taasisi mbali mbali zinazomilikiwa na kuendeshwa
na Kanisa Katoliki nchini Gambia pamoja na kukutana na wawakilishi wa Halmashauri
ya Walei, Mapadre na watawa kutoka Jimbo Katoliki Banjul.
Askofu mkuu Miroslaw
Adamczyk, Balozi wa Vatican nchini Gambia, alipata nafasi pia ya kuadhimisha Fumbo
la Ekaristi Takatifu kwenye Seminari ndogo ya Mtakatifu Petro, ambako kuna Waseminari
wadogo kumi na wawili wanaoendelea na majiundo yao ya Kikasisi. Hapa inaonekana kwamba,
kuna ukame wa miito, changamoto na mwaliko kwa waamini kusali ili kumwomba Bwana wa
mavuno aweze kupeleka watenda kazi wema na watakatifu katika shamba lake!