Viongozi wa kidini na wananchi wa Sudan ya Kusini katika ujumla wao wanasema wamechoka
na vita, wanataka kuona: usalama, amani na utulivu vikirejea tena Kusini mwa Sudan
ili watu waanza kuchakarika kujitafutia maendeleo! Falsafa ya vita kama suluhu ya
migogoro ya kisiasa haina mantiki wala mashiko kwa wananchi wa Sudan ya Kusini. Hivi
ndivyo wanavyosema viongozi wa kidini katika tamko lao lililochapishwa kwenye gazeti
la "Sudan Tribune".
Tangu machafuko ya kisiasa yajitokeze nchini humo hapo
tarehe 15 Desemba 2013, zaidi ya watu 1,000 wamekwisha kufariki dunia na wengine 200,
000 hawana makazi maalum baada ya kuzikimbia nyumba zao kwa kuhofia usalama wa maisha
yao.
Wananchi wanataka amani hivyo wanawaomba wadau mbali mbali wanaosaidia
kusuluhisha mgogoro huu kuhakikisha kwamba, pande zote mbili zinaweka silaha chini
na kuanza mazungumzo na wala machafuko haya ya kisiasa yasigeuzwe kuwa ni sababu ya
kuibuka tena vita vya kikabila nchini Sudan ya Kusini.
Wananchi wahamasishwe
kushinda kishawishi cha vita vya kikabila kwani huu ni mgogoro wa kugombania madaraka
ya kisiasa, unaotaka kulitumbukiza taifa katika maafa makubwa! Mazungumzo kati ya
pande zinazohusika yanaendelea mjini Addis Ababa, Ethiopia.