Upendo wa Kikristu si maigizo lakini ni ukarimu na wema halisi
Upendo wa Kikristo daima ni tabia yenye asili ya ukarimu na wema katika maisha ya
kila siku. Hivyo, ni upendo unaotenda zaidi kuliko maneno, ni zaidi katika kutoa
kuliko kupokea. Ni ujumbe wa Papa Francisko,katika homilia yake wakati wa Ibada ya
Misa Alhamis hii asubuhi, Ibada aliyo iongoza katika kanisa dogo la Mtakatifu Marta,
Vatican. Papa amesisitiza, hivyo upendo huo si mahaba ya juu juu lakini ni
upendo wa kina usio na choyo katika kutoa na kuwapokea wengine. Ni upendo wa mtu aliye
maskini lakini bado ana hamu ya kutaka kutoa hata kidogo alicho nacho kuliko yeye
kupokea, na hana la zaidi isipokuwa ni upendo wake kwa Kristo. Papa Francisko
alitoa mafundisho akitafakari barua ya kwanza ya Mtume Yohane , ambamo anasisitiza
na kurudia mara kwa mara, iwapo sisi tutapendana kati yetu, Mungu atabaki kuwa nasi
na Upendo wake mkalimilifu utakaa ndani mwetu. Papa ametaja uzoefu huu wa imani,
umo hasa katika nguzo mbili.
Nazo ni Sisi kuwa ndani ya Mungu na Mungu kukaa
ndani mwetu. Hayo ndiyo Maisha ya Mkristu . Na hivyo si kukaa katika roho wa malimwengu
, wala kukaa katika purukushani za maisha , wala kukaa katika ibada ya sanamu , wala
kukaa katika ubatili, lakini ni kukaa katika Bwana. Naye huungana nasi na kubaki ndani
mwetu. Lakini kuna sharti kwamba ni lazima kwanza sisi kukubali kubaki ndani mwake
ili nae aweze kubaki ndani mwetu . Bahati mbaya, mara kwa mara sisi binadamu tunapenda
kwenda mbali nae, tunashindwa kubaki ndani mwake.
Papa aliendelea kuweka
wazi tabia na mienendo ya roho wa upendo wa Kikristo, katika hali ya ubinadamu, kwamba,
kukaa katika upendo wa Mungu si tu huustarehesha moyo , lakini pia ni jambo jema
kulisikia na kuliishi.
Upendo wa Kikristo daima una thamani ya hali ya juu
na ni halisi. Upendo wa Kikristo ni ukweli. Yesu mwenyewe , wakati anazungumzia upendo,
hakueleza tu kwa maneno lakini alitenda, aliwalisha wenye wenye njaa , kutembelea
wagonjwa n.k, hivyo ni Upendo wa kweli. Na asiyekuwa na upendo huu, humezwa na ubinafsi
, siku zote akitafuta kupata faida zake mwenyewe , humezwa na roho wa kutoridhika,
na kuonekana tofauti na mwenye upendo wa Kristu ambaye hukaa na moyo wazi, katika
kumtumainia Mungu na Mungu huungana katika moyo huo kwa upendo wake Mkamilifu.