2014-01-09 08:42:22

Rais wa Ghana ameamua kula sahani moja na wala rushwa hadi kieleweke!


Askofu Osei Bonsu, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana amempongeza Rais John Dramani Mahama wa Ghana kwa kujifunga kibwebwe kupambana kufa na kupona na saratani ya rushwa ambayo imeenea katika medani mbali mbali za maisha nchini Ghana.

Maaskofu wanamtaka Rais Mahama "kula sahani moja" na watu waliotopea katika kutoa na kupokea rushwa mambo yanayopindisha haki msingi katika huduma za kijamii nchini Ghana. Ghana imeamua kuchukua hatua za makusudi kabisa ili kupambana na rushwa kwa kuwafikisha watuhumiwa wote mbele ya mkondo wa sheria. Rushwa imeota mizizi si tu katika masuala ya kisiasa bali hata katika nyanja nyingine za maisha.

Lakini, rushwa inanuka: mahakamani, kwenye masuala ya uchumi na kwa uchungu mkubwa anasema Askofu Bonsu kwamba, hata ndani ya Kanisa huko nako rushwa imebisha hodi! Mapambano dhidi ya rushwa ni jukumu la wananchi wote wa Ghana na wala si kwa Rais wa nchi peke yake! Wananchi watambue kwamba, rushwa ni adui wa haki, wakatae kutoa na kupokea rushwa, ili haki itendeke!







All the contents on this site are copyrighted ©.