Serikali ya Rwanda imeanza Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 20 tangu yalipotokea
mauaji ya kimbari nchini humo yaliyosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.
Maadhimisho haya yamezinduliwa na Rais Paul Kagame wa Rwanda aliyewasha mwenge
utakaokimbizwa nchi nzima kama kielelezo cha Maadhimisho ya Mauaji ya Kimbari nchini
Rwanda, kabla ya kuanza kipindi cha maombolezo ya kitaifa hapo tarehe 7 Aprili 2014.
Inakadiriwa
kwamba, watu laki nane waliuwawa nchini Rwanda kati ya Mwezi Aprili na Juni 1994,
wengi wao wakiwa wanatoka katika kabila la Watutsi. Televisheni ya taifa imeonesha
baadhi ya matukio haya ambayo kwa takribani siku mia moja tu, maelfu ya watu walikuwa
wamepoteza maisha na nchi kusambaratika kutokana na hofu za mashambulizi ya kikabila.
Miaka
ishirini imepita, Rwanda imeanza kujielekeza katika mchakato wa ukweli na upatanisho,
lakini wachunguzi wa mambo wanasema kwamba, kurasa chungu za mauaji ya kimbari bado
hazifutwa katika mawazo ya wananchi wengi wa Rwanda. Wapinzani wa Serikali ya Rais
Paul Kagame wanasema kwamba, bado anafanya hujuma kwa wapinzani wake, kwa kuwafutilia
mbali na wala hakuna watu wanaowajibishwa kutokana na mauaji hayo!