Mshikamano na wananchi wa Sudan ya Kusini katika kipindi hiki kigumu!
Shirika la Kitume Kimataifa la Pax Christi linapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati
na wananchi wote wa Sudan ya Kusini wakati huu wanapokabiliana na machafuko ya kisiasa
ambayo yamepelekea mauaji ya watu wasiokuwa na hatia na wengine wengi kulazimika kuyakimbia
makazi yao. Inasikitisha kuona kwamba, kinzani za kisiasa zinageuzwa na kupachikwa
masuala ya ukabila; mambo ambayo ni hatari sana kwa ustawi na maendeleo ya wengi.
Miaka
miwili iliyopita, Sudan ya Kusini iliadhimisha uhuru wake, kwa kutaka kukazia misingi
ya haki, amani, upatanisho na maendeleo ya wengi; demokrasia ikipewa msukumo wa pekee.
Lakini mwishoni mwa Mwaka 2013, demokrasia na uhuru wa wananchi wa Sudan ya Kusini
umegeuka kuwa ni maafa kwa watu wasiokuwa na hatia. Machafuko na kinzani za kisiasa
na kijamii zimepelekea watu kuyakimbia makazi yao, hali ambayo inakwamisha jitihada
za kujiletea maendeleo endelevu. Jumuiya ya Kimataifa inaonesha wasi wasi wake kutokana
na kuzuka kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan ya Kusini.
Taarifa zinaonesha
kwamba, kuna zaidi ya watu elfu moja wamekwishapoteza maisha kutokana na vita inayoendelea
Sudan ya Kusini. Mauaji ya watu kwa kisingizio chochote kile linasema Pax Christi
ni ukiukwaji wa haki msingi za binadamu. Kumbe, kuna haja kwa pande zote zinazohusika
na machafuko ya kisiasa nchini Sudan ya Kusini, kuketi kwa pamoja na kuanza mchakato
wa majadiliano yatakayosaidia kusitisha umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia.