Matumaini ya kupata chanjo dhidi ya Malaria kwa Mwaka 2014?
Kuna matumaini makubwa kwa Bara la Afrika katika kipindi cha Mwaka 2014 kuweza kupata
kinga dhidi ya ugonjwa wa Malaria ambao umekuwa ni tishio kwa maisha na maendeleo
ya wananchi wengi Barani Afrika. Majaribio ya chanjo yaliyofanywa kwa watoto 15, 500
yanaonesha kwamba, ugonjwa wa Malaria ulipingua kwa kipindi cha miezi 18 ya majaribio
ya chanjo hii mpya.
Kampuni ya GlaxosmithKline inatarajiwa kuwasilisha chanjo
hii kwa Taasisi ya Ulaya kwa uchunguzi wa kina kabla ya kuanza kuuzwa madukani. Chanjo
hii inaonesha mafanikio ingawa bado kuna mashaka kidogo yanayofanyiwa kazi na wataalam
wa chanjo. Takwimu za Shirika la Afya duniani zinaonesha kwamba, kwa Mwaka 2010 watu
waliofariki dunia kutokana na ugonjwa wa Malaria walikuwa ni 666, 000 na zaidi ya
watu millioni tatu walishambuliwa kwa ugonjwa wa Malaria duniani, hali ambayo inatishia
usalama wa maisha ya watu wengi duniani.
Waathirika wakubwa wa ugonjwa wa Malaria
ni watu wanaoishi Kusini mwa Jangwa la Sahara na Asia. Dawa nyingi zinazotumika dhidi
ya ugonjwa wa Malaria zimewafanya watu wengi kuwa sugu, jambo ambalo linahatarisha
usalama wa maisha ya watumiaji wa dawa hizi. Usafi wa mazingira pamoja na utumiaji
wa vyandarua vyenye dawa ni jambo muhimu sana katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa
Malaria duniani.
Upatikanaji wa chanzo ya ugonjwa wa Malari ni jambo la kutia
matumaini kwa watu wengi wanaoteseka kutokana na ugonjwa huu sehemu mbali mbali za
dunia. Wataalam wanasema, si jambo rahisi kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa Malaria
ambao umekuwa sugu kwa miaka mingi. Chanjo inayofanyiwa majaribio ni changamoto kwa
Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa kutaka kudhibiti ugonjwa wa Malaria duniani.