Wananchi wanateseka Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati!
Viongozi wa kidini Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa pamoja wametoa tamko kwa Jumuiya
ya Kimataifa kuunganisha nguvu katika kuokoa maisha ya wananchi wengi wanaokabiliwa
na hali ngumu kutokana na vita inayoendelea nchini humo. Inasikitisha kuona kwamba,
vita hii imegeuzwa kuwa ni vita ya kidini, hali ambayo imepelekea wananchi wengi kuyakimbia
makazi yao na hivyo kujikuta wanaishi katika makazi ya muda ambayo bado hayajaandaliwa
vyema!
Askofu mkuu Dieudonnè Nzapalainga wa Jimbo kuu la Bangui na Shiekh Omar
Kobine Layama, Imam mkuu wa Mji wa Bangui, kwa pamoja wanaomba Umoja wa Mataifa kupeleka
vikosi vya kulinda amani Jamhuri ya Afrika ya Kati, ili kuokoa maisha ya maelfu ya
watu ambayo kwa sasa yako hatarini. Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki yanaendelea
kuwahudumia wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi mjiji Bangui.