2014-01-06 09:17:33

Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar: baadhi ya mafanikio!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameisifu Zanzibar kuwa ni nyota inayong’ara ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria katika Afrika akisisitiza kuwa siyo tu kwamba, inaongoza katika Afrika lakini ni mfano wa kuigwa duniani. Aidha, Rais Kikwete ameisifu na kuipongeza Zanzibar kwa kuvuka lengo la Shirika la Afya Duniani (WHO) la kuhakikisha kuwa wananchi hawatembei umbali wa zaidi ya kilomita tano kufuata huduma ya afya. Zanzibar imeshuka kutoka umbali wa kilomita tano kama inavyopendekezwa na WHO hadi kufikia kilomita tatu.

Rais Kikwete pia amekisifu Kikosi Maalum cha Kupambana na Magendo (KMKM) cha Zanzibar kwa kazi nzuri ya kulinda mipaka ya majini na kudumisha utulivu ambao Tanzania imeushuhudia katika miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo kilele cha sherehe zake kitakuwa Jumapili ya Januari 12, mwaka huu, 2013.

Rais Kikwete amezungumza hayo Jumamosi, Januari 4, 2014, na mamia ya wananchi, maofisa na askari wa KMKM baada ya kuifungua rasmi hospitali kubwa na ya kisasa ya Kikosi hicho kwenye eneo la Kibweni mjini Zanzibar. Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya siku mbili ya kikazi katika Zanzibar amefungua rasmi hospitali hiyo ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za Sherehe ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akizungumzia mafanikio ya Serikali ya Mapinduzi (SMZ) katika miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika nyanja mbali mbali, Rais Kikwete amesema kuwa Zanzibar imekuwa na mafanikio makubwa na ya kujivunia katika kipindi hicho. Rais amesema kuwa moja ya mafanikio makubwa yamekuwa katika sekta ya afya ambako miongoni mwa mambo mengine Zanzibar imefanikiwa kufuta ugonjwa wa malaria Visiwani. “Haijawahi kutokea katika Afrika nchi yoyote ikafanikiwa kutokomeza ugonjwa wa malaria. Hapa Zanzibar imewezekana na kwa kweli kama siyo mlolongo wa masharti ya kimataifa, Zanzibar ingeweza tayari kutangaza kuwa Zanzibar imefuta malaria.”

Rais Kikwete alikuwa anazungumzia takwimu za Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Juma Duni Haji ambaye alikuwa amemwambia Rais Kikwete kuwa mwaka 2007, vifo vilivyotokana na ugonjwa wa malaria vilikuwa asilimia 3.1 lakini mwaka 2011 asilimia hiyo ilikuwa imeshuka hadi sifuri.

Mheshimiwa Haji amesema kuwa mwaka 2004/5, uwepo wa ugonjwa wa malaria katika Zanzibar ulikuwa asilimia 44.6 lakini mwaka juzi, 2012, asilimia hiyo ilikuwa imeshuka na kuwa chini ya asilimia moja. Kutokana na takwimu hizo, Rais Kikwete amesema: “Mafanikio ya Zanzibar katika kukabiliana na malaria hayajawahi kufikiwa na nchi yoyote katika Afrika. Zanzibar ni nyota inayong’ara katika kukabiliana na ugonjwa wa malaria.”

Hata hivyo, Rais Kikwete ameonya kuwa ni muhimu kwa Zanzibar kuendelea kudumisha hatua zote ambazo zimeleta mafanikio hayo vinginevyo “tutarudi nyuma kama ilivyopata kutokea huko tulikotoka. Hii ni mara ya tatu kwa Zanzibar kufikia hatua nzuri kiasi hiki. Nataka tudumishe hali hii iwe ya kudumu siyo kurudi nyuma kama iliyopata kutokea mara mbili nyuma.”

Kuhusu mafanikio ya Zanzibar ya kupunguza masafa ya wananchi wake kupata huduma angalau kufikia kilomita tatu, Mheshimiwa Haji amesema: “Kwa furaha kubwa, naomba kukueleza wewe Mheshimiwa Rais pamoja na wageni wetu kuwa Zanzibar imefanikiwa kufikia lengo hili kwa muda mrefu sasa na kulipindukia. Hakuna mwananchi wa Zanzibar anayesafiri zaidi ya kilomita tatu kutoka kituo kimoja cha afya kwenda kingine.”

Rais Kikwete amepongeza hatua hiyo akisisitiza kuwa mafanikio hayo katika afya kama ilivyo katika sekta nyingine ni ushahidi usiopingika wa usahihi wa Mapinduzi ya Januari 12, mwaka 1964, kwa sababu mapinduzi yalikuwa na shahaba ya kuleta maendeleo kwa kuwaondoa wale ambao walikuwa hawatafuti maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.








All the contents on this site are copyrighted ©.