2014-01-04 09:37:07

Viongozi 22 wa Kanisa waliouwawa kikatiliki katika Kipindi cha Mwaka 2013


Katika kipindi cha Mwaka 2013 kuna viongozi wa Kanisa 22 wameuwawa kikatiliki duniani kote wakiwa wanatekeleza utume wao wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Idadi hii imeongezeka maradufu ikilinganishwa na Mwaka 2012, kadiri ya takwimu zilizokusanywa na Shirika la Habari za Kimissiomari la Fides.

Mwaka 2013 umefungwa kwa mauaji ya Padre Eric Freed, Paroko wa Parokia ya Eureka, nchini Canada, aliyeuwawa katika mkesha wa Mwaka Mpya 2014. Jeshi la Polisi nchini Canada linaendelea na uchunguzi ili kubainisha chanzo na sababu za mauaji hayo!

Amerika ya Kusini kwa kipindi cha miaka mitano sasa linaongoza kwa mauaji ya viongozi wa Kanisa, Nchi ya Colombia ikiwa ni kinara cha mauaji haya. Mapadre 19 wameuwawa kikatili huko Amerika ya Kusini; mtawa mmoja na waamini walei wawili. Bara la Amerika limemwaga damu ya viongozi wa Kanisa kumi na mmoja; Saba kutoka Colombia na wanne wameuwawa nchini Mexico na mmoja mmoja kutoka Brazil, Venezuela, Panama na Haiti.

Mauaji ya viongozi wa Kanisa, Tanzania pia imeingia pia katika orodha hii kwa mauaji ya Padre Evaristi Mushi, kutoka Jimbo Katoliki la Zanzibar, aliyeuwawa kikatili wakati anajiandaa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Taarifa zinazonesha kwamba, kama si ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu, bomu lililolipuliwa Jimbo kuu la Arusha lingeweza kusababisha maafa makubwa!

Huko Madagascar Sr. Marie Emmanuel Helesbeux, aliuwawa kwa kupigwa na hatimaye kunyongwa kikatiliki. Nchini Nigeria, Afra Martineli, mlei, alikutwa amefariki dunia nyumbani kwake kwa kukatwa katwa mapanga! Haya yote ni mauaji ya kutisha, lakini ni mbegu ya Ukristo sehemu mbali mbali za dunia.

Barani Asia, Padri mmoja aliuwawa kikatiliki huko India, Syria na mwamini mlei mmoja alipoteza maisha yake huko nchini Ufilippini. Barani Ulaya, Padre mmoja aliuwawa nchini Italia. Kanisa bado linaendelea kuonesha wasi wasi kutokana na baadhi ya viongozi wa Kanisa waliotekwa au kupotea katika mazingira ya kutatanisha na hadi sasa hawajulikani mahali walipo.

Majadiliano ya kidini na kiekumene; ukweli na haki; amani na utulivu; uhuru wa kuabudu na hali ya kuvumiliana ni mambo msingi katika mchakato wa kusitisha na kuzuia mauaji ya watu wasiokuwa na hatia kwa chuki za kidini au kwa dhana tu ya kutaka kukumbatia utamaduni wa kifo!







All the contents on this site are copyrighted ©.