2014-01-04 14:23:48

Umuhimu wa Baba katika maisha mchanganyiko kifamilia


Karibu mpendwa msikilizaji katika kipindi dunia Mama ambamo tunaendelea kuichambua mada Maisha Mchanganyiko katika kijamii, tukiwa ndani ya familia, hasa kwa nyakati hizi ambamo akili zetu bado zimemezwa na tukio la kifamilia la sherehe za kuzaliwa mkombozi wetu Yesu Kristu katika familia ya kibinadamu ya Maria na Yosef.

Katika makala yaliyopita, uchambuzi yakinifu wa kisayansi, ulituonyesha kwamba , mwanamke ameumbwa na asili ya kuwa mama, kutunga mimba kama matokeo ya muungano wa ndoa na mtu mme na mtu mke. ikiendana sambamba na muundo wa kisaikolojia na kimwili kwa wanawake. Na kumbe mtu mke anamhitaji mwenza mme(baba ) katika kufanikisha ukamlifu wa upendo wao. Leo nawaalika turejeshe mawazo yetu katika kuona wajibu wa Baba ndani ya Familia.

Baba kama inavyojulikana tangu kuumbwa kwa dunia, ni mkuu wa familia, kama neno la Mungu, linavyotuambia: Mwenyezi Mungu alimuumba mwanamme kwanza, kutoka katika mavumbi ya aridhi, akampulizia pumzi hai na huyo mwanamme akawa kiumb e hai. Mungu alimtwaa huyo mwanaumme na kumweka katika bustani ya Edeni ailime na kuitunza ( Mwanzo 2). Hivyo mwanamme alikabidhiwa moja kwa moja jukumu hili la kuwa mtunzaji wa walio chini ya himaya yake.

Katika kuona ukuu wa wajibu huu, kwa namna moja au nyingine, jamii ilitafuta namna ya kuuenzi ukuu wa mwanaume au baba kama historia ya maisha ya kijamii inavyo onyesha katika baadhi ya mataifa, huwa na siku maalum ya kumuenzi baba kutambua ukuu wake wa kibaba na umuhimu wake katika familia na ukuu wa mababa katika jamii.

Mataifa hayo huwa na sherehe maalum za kumuenzi Baba,ambamo maandishi yameonyesha wengi hufanya hizyo katika Jumapili ya tatu ya mwezi Juni, ingawa pia mataifa mengine huisherehekea siku hii ya baba, sambamba na Siku Kuu ya Kupaa Bwana mbinguni, siku arobaini baada ya Siku Kuu ya Pasaka, kama ilivyo katika taifa la Ujeruman, ambayo inapewa uzito wa siku ya mapumziko ya kitaifa. Siku hii inapaswa kuwa ni siku ya mapumziko ya wanaume watu wazima, kukutana kama marafiki, kubarizi na kufurahia pamoja kama baba wa familia, kula na kunywa, kuufurahia ubaba wao.

Lakini umaarufu wake uliojitikeza katika karne ya 17-18, ulianza kupungua zaidi katika karne ya 20, kutokana na wanaume wengi kukerwa na jinsi wenzi wao walivyoitumia vibaya siku hii ya Baba wakiigeuza kuwa siku ya ulevi na makelele yasiyokuwa na maana mitaani. Hivyo baba wengi hawakuona tena maana ya kuwa na siku hiyo.

Hata hivyo , adhimisho hili inaendelea kuwepo katika hali ya kimyakimya katika baadhi ya mataifa ya Ulaya. Barani Afrika, ni kama haipo, husikika kidogo kwa mbali nchini Kenya ambako nako si siku ya kitaifa.

Inaeleweka wazi, katika miaka ya nyuma, wajibu wa baba nyumbani ulifahamika zaidi kuwa ndiye mfanikishaji wa mahitaji ya nyumbani tangu upatikanaji wa chakula na fedha na maendeleo nyumbani, hata akina mama walisadiki hilo. Lakini kwa sasa utamaduni huo umebadilika. Familia nyingi kwa wakati huu, wote baba na mama ni watafutaji wa mahitaji ya familia.
Watalaam wa sayansi ya jamii wanaonya mabadiliko hayo yasipunguze majukumu ya baba katika familia, kama alivyoandika Profesa Louis WEiss, katika makala yake juu ya wajibu wa baba katika maisha ya kwanza ya mtoto. Katika kipindi cha miaka 1940-1970, wakati wa mapambazuko ya wanawake kudai haki sawa na wanaume katika maisha ya kijamii, wakati kulipoibuka kwa kishindo vyama vya wanawake kulilia haki ya kuwa watu huru kama wenzi wao wanaume, na kukataa ugandamizwaji uliokuwa ukifanywa na wanaume dhidi yao, ilileta hoja kwa watalaam katika masuala ya kijamii, kutazama kwa makini kishindo cha mabadiliko haya katika mifumo ya kijamii.

Na hasa walitazama jinsi utendaji majukumu ya wanafamilia yanavyoweza kuathiriwa ka mabadiliko haya hasa uwezo wa kujipatia fedha ya ziada na jinsi ya kugawana majukumu katika maisha ya nyumbani, ikiwemo kuelea watoto. Watalaam hao waliweza kuona kwa uwazi zaidi, umuhimu wa baba kama mleta mkate, mlezi na mfanikishaji wa majiundo kwa lika la watu vijana kama alivyoandika Michael Lamb katika makala yake ya wajibu wa baba katika maeendeleo ya mtoto(1980).
Tafiti nyingi za kisayansi, zimethibitisha umuhimu wa uwepo wa baba katika matokeo ya makuzi ya watoto, hasa watoto kujenga tabia ya kuwa thabiti katika maamuzi na kujizuia au kujinyima. Tafiti hizo zinasema , mtoto huiga kutoka kwa baba yake jinsi ya kuwa imara katika kufanya maamuzi na hasa katika kujinyima, kwa ajili ya jambo la muhimu, lifanyike kwanza, kama vile kazi za shule au kazi za nyumbani, ingawa pia mama analiweza jukumu hili, lakini baba huwa na mkazo zaidi katika suala hili
Upendo wa baba kwa mtoto
Pia wanasaikolojia wanasema, jukumu la upendo wa baba katika maendeleo ya mtoto lina umuhimu mkubwa katika kusaidia majiundo ya mtoto kwa kadri anavyokua kimwili , kiakili, na kijamii. Mambo mengi ya baba katika mahusiano yake ya kijamii pia huwa ni kioo katika makuzi ya mtoto kama walivyoeleza Radin & Harold - Goldsmith(, 1989 ) waliandika katika kitabu chao, juu umuhimu wa Baba kuwa na muda wa kukaa na Mtoto wake.

Wanasema, kuna madhara, pale baba anapokosa muda wa kukaaa na mwanae, hasa katika kujali maendeleo ya akili ya mtoto, kwenye umri kati ya miaka 6-11, ambacho ni kipindi cha kwanza cha masomo shuleni. Utafiti mwingine pia unataja madhara ya kukosekana kwa upendo wa mzazi mmoja wakati wa uchanga kwamba, hata katika maisha ya baadaye ya mtoto huwa na mwelekeo wa mtoto kupendelea upande mmoja tu.

Aidha tafiti zinasema, upendo wa Baba pia umeonyesha umuhimu mkubwa katika maendeleo ya makuzi ya mtoto kiakili na kitabia, kwamba, tabia ya mtoto inaweza kutambirika kwa urahisi zaidi kutokana na upendo wa Baba kuliko upendo wa mama. Ukaribu kati ya baba na mwanae huchangia furaha ya mtoto, na pia matatizo ya kitabia, na hasa kisaikolojia kuliko yalivyo mahusiano ya mama na mtoto ( Rohner , 1998) katika makala yaliyo lenga kuonyesha jinsi upendo wa kina wa baba,unavyokuwa na na mahusiano kwa watoto, kisaikolojia , afya, na katika matatizo ya kitabia, ikionyesha umuhimu wa baba katika jukumu la kufanikisha maendeleo ya mtoto.

Matokeo ya tafiti katika sayanasi ya kijamii yanaendelea kuonyesha uwepo wa baba katika familia, huwa ni somo kwa watoto, katika jinsi ya kuwa na mahusiano thabiti ndani ya familia. Pale baba anaposhughulikia maisha ya baadaye ya watoto wake kwa moyo wa upendo na majitoleo binafsi ya kina, watoto ingawa huonekana kama vile hawajali kumbe huliona hilo na kujifunza, kuwa na huruma zaidi katika maisha ya kijamii. Na pia imeonekana mwingiliano huo wa maisha ya utotoni ndani ya familia hujenga tabia ya muda mrefu kwa watoto, ikiwemo hali ya maisha ya ndoa zao wenyewe na katika kujali pia maisha ya baadaye ya watoto wao.

Katika mtazamo huo, kumbe kila baba anakuwa ni kiungo muhimu katika upitishaji wa tabia njema kwa watoto wake na katika ujenzi wa mahusiano ya mtoto kisaikolojia, kielimu na kijamii.
Kwa umuhimu huu wa baba katika maisha ya mtoto na jamii kwa ujumla, tunauona umuhimu wa kuwaenzi baba wote duniani.
Makala imeandaliwa nami TJ Mhella.








All the contents on this site are copyrighted ©.