2014-01-04 11:28:20

Jengeni amani, udugu na mshikamano Mashariki ya Kati!


Nchi Takatifu inahitaji umoja na mshikamano wa kidugu kati ya waamini wa dini ya Kiislam, Kiyahudi na Kikristo na kwamba, kuna idadi kubwa ya watu wenye mapenzi mema wanaendelea kuchakarika usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba, haki, amani, udugu na mshikamano vinaimarishwa huko Mashariki ya Kati. Lengo ni kusimama kidete ili kulinda na kudumisha haki na amani kwa watu wote katika Nchi Takatifu.

Ni changamoto iliyotolewa na Patriaki Fouad Twal wa Yerusalem wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria, Mama wa Mungu, sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 47 ya Kuombea Amani kwa Mwaka 2014. Wito na dhamana ya Wakristo ni kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kutoa huduma ya upendo na mshikamano kwa watu wote wanaokutana nao, ili kujenga na kuimarisha udugu wa kweli.

Hili ndilo jukumu linalotekelezwa na Mashirika ya Misaada Kitaifa na Kimataifa yaliyoko chini ya mwamvuli wa Kanisa Katoliki huko Mashariki ya Kati. Ni huduma ya upendo inayotekelezwa na Mashirika ya Kitawa katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu; kiasi kwamba, hiki kimekuwa ni kielelezo cha ushuhuda wa imani katika matendo!

Patriaki Twal anasema, udugu ni msingi na njia ya amani kama kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya 47 ya Kuombea Amani Duniani inayoelekeza kwani binadamu wote wanapaswa kutambua kwamba, wao ni watoto wa Mwenyezi Mungu hivyo wanahamasishwa kujenga na kudumisha udugu miongoni mwao, kwa kuheshimiana na kuthaminiana. Haya ndiyo matumaini yanayoletwa na Yesu Kristo Mfalme wa Amani huko Mashariki ya Kati, eneo ambalo kwa miaka mingi limeandamwa kwa matukio ya vita, kinzani na migogoro ya kijamii na kisiasa.

Patriak Twal anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujenga na kuimarisha amani na haki jamii inayosimikwa katika misingi ya imani, ukweli na upendo. Kama waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuwashirikisha jirani zao ile Injili ya Furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Udugu ujenge ushirikiano na mshikamano wa dhati, daima wakisimama kidete kutafuta, kulinda na kudumisha mafao ya wengi.

Patriak Twal anasema, familia ni msingi na nguzo thabiti katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Hapa ni mahali pa kwanza kabisa katika ujenzi wa udugu, umoja na mshikamano. Patriak Twal anawatakia waamini maandalizi mema katika Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia inayotarajiwa kuadhimishwa Mjini Vatican mwezi Oktoba, 2014.

Hata katika kinzani na changamoto za utandawazi, Kanisa halina budi kutafuta majibu muafaka ili kuzima kiu na njaa ya watu wa ndoa na familia katika Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo; kwa kutambua kwamba, Familia ni mdau mkubwa katika azma ya Uinjilishaji Mpya. Jumuiya za Kikristo hazina budi kuzivalia njuga changamoto za kifamilia, ili kweli familia iendelee kuwa ni shule ya haki, amani, upendo na mshikamano; mahali pa kuonjeshana huruma na upendo.









All the contents on this site are copyrighted ©.