2014-01-04 09:04:54

Idadi ya Makardinali kwa sasa ni 200, kati yao 107 wana haki ya kupiga na kupigiwa kura wakati wa uchaguzi wa Papa Mpya!


Takwimu za Kanisa Katoliki zinaonesha kwamba, hadi kufikia tarehe Mosi, Januari 2014, kulikuwa na jumla ya Makardinali 200, kati yao kuna Makardinali 107 wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura wakati wa uchaguzi wa Papa Mpya. Wengine 93 hawana haki tena ya kupiga wala kupigiwa kura. Hawa ni wale Makardinali ambao kati yao 2 walioteuliwa na Papa Paulo wa VI; Makardinali 118 waliteuliwa na Mwenyeheri Yohane Paulo II na wengine 82 wameteuliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI.

Kanisa Marekani ya Kaskazini, lina jumla ya Makardinali 26, kati yao wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura ni 16. Amerika ya Kati ina jumla ya Makardinali 4 kati yao, Makardinali 3 ndio wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura. Amerika ya Kusini ina jumla ya Makardinali 21, wote wana haki ya kupiga na kupigiwa kura.

Takwimu za Bara la Afrika zinaonesha kwamba, kuna jumla ya Makardinali 17, kati yao wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura ni 11. Idadi ya Makardinali Barani Asia kwa sasa ni Makardinali 19 kati yao Makardinali 11 tu ndio wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura. Oceania kwa upande wake, lina jumla ya Makardinali 4, kati yao ni Kardinali mmoja tu ndiye mwenye sifa na haki ya kupiga kura wakati wa kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Bara la Ulaya linaongoza kwa kuwa na Makardinali 109, kati yao kuna Makardinali 56 wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura wakati wa uchaguzi wa Papa Mpya. Kwa ufupi hii ndiyo picha halisi ya Makardinali ndani ya Kanisa ambao kimsingi ni wasaidizi na washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maisha na utume wake kwa Kanisa la kiulimwengu. Mwezi Februari 2014, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuteuwa Makardinali wengine wapya!







All the contents on this site are copyrighted ©.