2014-01-03 11:45:05

Simameni kidete kupambana na umaskini wa hali na kipato!


Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury na Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani katika ujumbe wake kwa Mwaka Mpya 2014 anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Uingereza kushikamana kwa pamoja dhidi ya umaskini wa hali na kipato unaoendelea kuongezeka kwa kasi nchini Uingereza katika miaka ya hivi karibuni! Mapambano haya yaanza kushika kasi kuanzia kwenye familia na maeneo ambamo wanaishi

Uinjilishaji wa kina unapania kumkomboa mtu mzima: kiroho n akimwili, kumbe Kanisa haliwezi kujikita tu katika utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu, bila kuangalia shida na mahangaiko ya watu wanaowahubiria; kwa kuwashirikisha upendo wa Mungu unaopaswa kujionesha pia kwa njia ya ushuhuda wa upendo kwa Mungu na jirani, lakini zaidi wale wanaoteseka na kusukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana na hali yao ya maisha. Watu wanataka kuwa na uhakika wa usalama na maisha yao na wanatamani kuona kwamba, Jamii inaishi katika misingi ya haki na amani.

Askofu mkuu Welby anasema, Kanisa liko mstari wa mbele kuhusiana na masuala ya kijamii kwani linatambua kwamba, limepokea upendo kutoka kwa Mwenyezi Mungu, unaowasukuma kuwashirikisha pia jirani zao. Hili si suala la kisiasa bali ni upendo. Mwanzoni mwa Mwaka, watu wana mipango na mikakati ya maisha, lakini kwa Mwaka 2014, kila mwamini apanie kuhakikisha kwamba, anashiriki katika mchakato wa maboresho ya hali ya maisha ya watu wanaomzunguka kwa kusimama kidete dhidi ya umaskini wa hali na kipato.

Hayati Mzee Nelson Mandela aliwahi kusema kwamba, mapambano dhidi ya umaskini si kitendo cha huruma bali ni sehemu ya mchakato wa haki jamii. Kila kizazi kinapaswa kufurahia mafanikio yanayopatikana kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Leo hii kuna mamillioni ya watu anasema Askofu mkuu Welby wanaoendelea kutumbukizwa kwenye umaskini wa hali na kipato. Kumbe, kila mtu anapaswa kushiriki kikamilifu katika mchakato dhidi ya umaskini, mahali anapoishi!







All the contents on this site are copyrighted ©.