2014-01-03 11:27:28

Mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato nchini Marekani


Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Marekani, kwa Mwezi Januari 2014 linaendesha kampeni dhidi ya umaskini nchini Marekani, kwa kujikita zaidi na zaidi katika kuhamasisha mikakati ya maendeleo endelevu, itakayosaidia mchakato wa mapambo dhidi ya umaskini wa hali na kipato nchini Marekani.

Juhudi hizi zinafanywa kwenye Parokia mbali mbali nchini marekani, kwa kuhakikisha kwamba, kila Parokia inajitahidi kusoma alama za nyakati kwa kuangalia hali ya umaskini wa watu wake, ili hatimaye, kuibua mbinu mkakati utakaofanyiwa kazi na Kanisa Katoliki nchini Marekani. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna watu millioni 46.5 nchini Marekani wanaoishi katika hali ya umaskini. Hawa ni sawa na asilimia 15% ya idadi ya wananchi wote wa Marekani.

Umaskini huu ni mlolongo wa matatizo yanayowakabili wageni na wahamiaji; ukosefu wa fursa za ajira mambo ambayo yanadhalilisha utu na heshima ya binadamu na kwamba, myumbo wa uchumi kimataifa unaendelea kusababisha majanga mbali mbali nchini humo!

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha moyo wa upendo na mshikamano kwa wale wote wanaoteseka kutokana na umaskini wa hali na kipato, ili wao pia waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya ushuhuda unaotolewa na watu wenye mapenzi mema.

Wananchi wa Marekani hawana budi kuunganisha nguvu zao ili kupambana na umaskini wa hali na kipato; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha pamoja na haki msingi za binadamu. Maaskofu wanakumbusha kwamba, tarehe 21 Januari 2014, Kanisa Katoliki nchini Marekani litafanya kesha kwa ajili ya kuwaombea watoto ambao hawajazaliwa; watoto ambao wanapaswa kulindwa na kutunzwa tangu pale wanapotungwa mimba tumboni mwa mama zao, hadi mauti ya kawaida yanapowafika kadiri ya mpango wa Mungu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linapenda kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Baba Mtakatifu Francisko kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini katika mikakati, mipango na maisha ya Makanisa mahalia, ili kuonesha upendo na mshikamano wa dhati. Maaskofu wanawahimiza waamini walei kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maisha ya hadhara, ili waweze kuchangia katika ustawi na maendeleo yao: kiroho na kimwili, lakini zaidi katika mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato!







All the contents on this site are copyrighted ©.