Siku kuu ya Jina takatifu la Yesu, Wayesuit kumwimbia Mungu utenzi wa shukrani kwa
ajili ya neema za Mtakatifu Pietro Favre!
Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Jina Takatifu la Yesu,
hapo tarehe 3 Januari 2014 anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa
la Yesu lililoko mjini Roma majira ya asubuhi, kama shukrani kwa neema na baraka kutoka
kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kutangazwa kwa Mwenyeheri Pietro Favre kuwa Mtakatifu.
Padre Adolfo Nicolàs
katika barua yake ya shukrani kwa Mama Kanisa kumtangaza Mwenyeheri Pietro Favre kuwa
Mtakatifu; uamuzi uliofanywa na Papa Francisko kwa kufuata sheria mlingano anasema,
Mtakatifu Favre awe ni changamoto na mfano wa kuigwa kwa Wayesuiti mmoja mmoja na
katika ujumla wao, katika hija ya mabadiliko ya maisha ya kiroho. Hili ni tukio
ambalo linafuatia tukio jingine kubwa la kihistoria la mabadiliko makubwa yaliyofanyika
kunako mwaka 1814, changamoto ya kuendelea kujikita katika maisha ya imani kwa Mwenyezi
Mungu, daima wakijitahidi kuwa ni wakweli na watu wazi; kwa kujitoa bila ya kujibakiza
kwa ajili ya Mungu na jirani! Ni Mtakatifu ambaye ameacha urithi wa kudumu katika
Shirika la Wayesuit. Mtakatifu Favre ni kati ya wafuasi wa Mtakatifu Inyasi kama vile
alivyokuwa Mtakatifu Francisko Xsaveri. Kwa miaka mitano wakawa pamoja kwenye Chuo
Kikuu cha Paris, Ufaransa na kushiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu, hapo tarehe 15
Agosti 1534. Wakati Mtakatifu Inyasi alipokuwa anakwenda nyumbani kwao Azpeitia,
Mwezi Machi 1535, akaacha Shirika mikononi mwa Jaalim Pietro Favre, ili kuliendeleza:
kiroho na kimwili. Akaonesha moyo wa udugu na urafiki, tayari kuanza mchakato wa ujenzi
wa Jumuiya ya Wayesuit, kama mahali pa kukutana na kuzungumza na Mwenyezi Mungu. Mtakatifu
Favre alikuwa ni mtu wa sala, aliyetajirisha maisha yake kwa njia ya sala na Ibada
kwa Bikira Maria, bila kuwasahau watakatifu na wafiadini. Ni mtu aliyesali kwa
ajili ya Kanisa, Viongozi na Shirika lake. Akawakumbuka waliotopea katika ukanimungu
bila kuwasahau waliokuwa wananyanyaswa na kuteswa kutokana na imani yao kwa Kristo
na Kanisa lake. Ni Mtakatifu aliyeamini katika maisha ya sala kama njia muafaka ya
kukutana na kuzungumza na Mwenyezi Mungu. Yesu Kristo akawa ni msingi na nguzo ya
maisha na utume wake ndani ya Kanisa. Hali ambayo ilijionesha kwa namna ya pekee katika:
Katekesi, Maandiko Matakatifu,Mahubiri. Mafundisho na Huduma kwa Jirani. Padre
Adolfo Nicolàs anasema, Mtakatifu Pietro Favre ataendelea kukumbukwa kama Kaka yao
mkubwa na kwamba, uwepo wake endelevu ndani ya Shirika ni baraka na neema kutoka kwa
Mwenyezi Mungu. Ni kielelezo cha utii na unyenyekevu kwa ajili ya Kristo na Kanisa
lake.