2014-01-02 11:41:46

Changamoto kwa Serikali na wadau mbali mbali nchini Uganda kutoa ufumbuzi wa kero za wananchi na kumong'onyoka kwa maadili na utu wema!


Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda, linaiomba Serikali ya Uganda kwa Mwaka 2014 kuweka mikakati madhubuti zaidi kwa ajili ya kushughulikia matatizo na kero za wananchi wa Uganda, kwani zisipopewa ufumbuzi wa kudumu, zinaweza kusababisha majanga ya kitaifa!

Kuna haja ya kukuza na kudumisha utawala bora, kupambana fika na utumwa mamboleo, unaoendelea kuwatumbukiza watu wengi katika biashara ya ngono na ushoga! Bado kuna kinzani na mivutano katika uwanja wa kisiasa, hali ambayo kimsingi inaweza kuhatarisha misingi ya haki, amani na utulivu wa kitaifa.

Askofu mkuu Cyprian Kizito Lwanga wa Jimbo kuu la Kampala katika mahojiano maalum na gazeti la "The Observer" anasema, kero hizi zisipopatiwa ufumbuzi wa kudumu, matokeo yake ni mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, uvunjaji wa haki msingi za binadamu na ukosefu wa utawala bora unaozingatia kanuni na sheria za nchi. Kuna haja ya kuwa na viongozi bora wanaoheshimu na kuzingatia kanuni na maadili ya kazi zao, daima wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao na maendeleo ya wananchi wote wa Uganda!

Wananchi wa Uganda wanapaswa kuwa makini dhidi ya vitendo vinavyopelekea kumong'onyoka kwa maadili na utu wema, kwa kisingizio cha uhuru na demokrasia. Vijana wasipojenga nidhamu na maadili kuhusiana na masuala ya ngono, kuna hatari ya kuwapoteza vijana hawa kwa siku za usoni. Viongozi wa kisiasa wawe makini kupambana na rushwa na ufisadi mambo ambayo yanaonekana kuwa ni sehemu ya vinasaba vya baadhi ya wananchi, kwani dhamiri imekufa! Mtu haoni kinyaa kupokea wala kutoa rushwa!

Demokrasia na uwakilishi wa wananchi wa Uganda Bungeni ni jambo ambalo linapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa, kwani ni jambo la kushangaza nchi kama Uganda kuwa na Wabunge 300! Kuna haja ya kupunguza viti vya wabunge kadiri ya uwezo wa walipa kodi na fedha hiyo ielekezwe katika maboresho ya maisha ya wananchi walio wengi. Ukosefu wa waalim bora, migomo ya mara kwa mara ni jambo ambalo Serikali ya Uganda pamoja na wadau wa elimu wanapaswa kuliangalia, ili kuwajengea wanafunzi uwezo wa kupambana na mazingira yao kikamilifu.

Askofu mkuu Cyprian Kizito Lwanga anasema kwamba, walimu wamechangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi na maendeleo ya nchi ya Uganda, kumbe, hili ni kundi ambalo linapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa!







All the contents on this site are copyrighted ©.