Wekezeni kwenye tunu msingi za kimaadili na utu wema ili kupambana na majanga ya kumong'onyoka
kwa maadili!
Kardinali Paul Poupard, Rais mstaafu wa Baraza la Kipapa la Utamaduni anasema, ili
kukabiliana na majanga yanayotokana na kumong’onyoka kwa tunu msingi za utu na maadili
mema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inawekeza zaidi na zaidi
katika tunu msingi za kimaadili kwa njia ya elimu makini.
Vijana wafundwe
kutambua na kuthamini tunu msingi za maisha ya adili na utu wema badala ya kung’ang’ania
haki ambazo wakati mwingine zinasigana na maadili. Ni changamoto ambayo imetolewa
hivi karibuni na Kardinali Paul Poupard mjini Paris, Ufaransa wakati akichangia mada
kwenye warsha iliyokuwa imeandaliwa na Taasisi ya Robert Schuman kwa ajili ya Ulaya,
wakati wa Kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu alipofariki Bwana Schuman ambaye ni kati ya
waasisi wa Umoja wa Ulaya.
Bara la Ulaya lilibarikiwa kuwa na tunu msingi
za maisha ya kiutu, kiroho na kijamii, lakini kadiri siku zinavyokwenda mbio anasema
Kardinali Poupard, mambo yanakwenda mrama! Jambo la kushangaza ni kuona kwamba, kuna
baadhi ya wanasiasa wanapenda kuridhisha kundi la watu wachache, kwa ajili ya mafao
yao binafsi, huku kilio cha wengi kuhusu: fursa za ajira na matarajio ya watoto wao
kwa siku za usoni, hayasikilizwi wala kushughulikiwa.
Mabadiliko kutoka katika
Jumuiya ya Ulaya na kuelekea Umoja wa Ulaya yamesababisha wananchi wa Bara la Ulaya
kuzamisha Meli ya mshikamano na upendo na kung’angania Meli ya umoja wa kiuchumi,
ambayo kwa sasa kimekuwa ni kilio cha wengi kutokana na athari za myumbo wa uchumi
kimataifa. Mshikamano wa dhati, mafao ya wengi ni kati ya vipaumbele vilivyotolewa
na waasisi wa Umoja wa Ulaya, kwa wakati huo. Inasikitisha kuona kwamba, ubinafsi,
upweke na mafao binafsi yanapigiwa debe zaidi kuliko hata mambo msingi yanayowaunganisha
wananchi wa Bara la Ulaya na jirani zao.
Wananchi wengi Barani Ulaya hawaridhiki
na mwenendo wa maisha kwa sasa. Kuna malalamiko mengi yanayowafanya watu kuanza kukata
tamaa ya maisha hasa kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa: hasa ukosefu
wa fursa za ajira ambalo kwa sasa limekuwa ni janga la wananchi wengi Ulaya; wafanyabiashara
wanakata tamaa na kuanza kufunga shughuli za uzalishaji mali hali ambayo inawanyima
vijana wengi kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.
Kodi na mapungufu
yake; rushwa na ufisadi, mmong’onyoko wa maadili na utu wema miongoni mwa viongozi
wa kisiasa ni kati ya mambo ambayo yanawachanganya wananchi wengi Barani Ulaya. Watu
wamekosa imani na masuala ya kisiasa kwani huko wanaingia watu kwa ajili ya kutafuta
masilahi binafsi. Mambo yote haya yamepelekea watu kukosa imani na wanasiasa pamoja
na serikali zao, kiasi kwamba, migomo na maandamano dhidi ya Serikali ni mambo ambayo
yamekuwa ni chakula cha kila siku kwa wananchi wengi.
Kardinali Paul Poupard
anasema, kuna haja kwa Bara la Ulaya kutafuta tena utambulisho na sura mpya katika
masuala ya kiuchumi, kifedha na kisiasa, kwani ile ndoto ya ufanisi katika utawala
inazidi kutoweka siku hadi siku katika Jumuiya ya Kimataifa kama inavyojionesha hata
kwenye Umoja wa Mataifa.
Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwekeza katika elimu
na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya, kwani wao ndio waathirika wakubwa wa
ukosefu wa fursa za ajira na mmong’onyoko wa maadili na utu wema.