2014-01-01 08:51:52

Papa Francisko atembelea Pango la Noeli mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni mwa Mwaka 2013, mara baada ya kuongoza Masifu ya Jioni kwa ajili ya Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu, kuimba utenzi wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, Te Deum na hatimaye, kufanya Ibada ya Kuabudu Ekaristi takatifu, aliondoka na kwenda kutembelea Pango la Noeli, lililoko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican.

Uwanja huu ulikuwa unatumbuizwa na Bendi ya Muziki ya Askari kutoka Uswiss waliokuwa wamevaliwa kwa unadhifu mkubwa, huku wakipita kwa maringo, utadhani kwamba, huku duniani mambo yote yote "ni maji kwa glasi". Itakumbukwa kwamba, Pango Noeli kwa Mwaka 2013 ni zawadi kutoka Jimbo kuu la Napoli kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Baba Mtakatifu alipofika kwenye Pango la Noeli alisali kwa kitambo na baadaye alianza kusalimiana na mafundi waliotengeneza Pango la Noeli kwa Mwaka 2013. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza kwa ubinifu na ufundi mkubwa walioutumia kwa ajili ya kutengeneza Pango hili likaonekana kama lilivyo.

Baba Mtakatifu alipata pia nafasi ya kusalimiana na waamini waliokuwa wamefika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kusali ili kufunga Mwaka wa Serikali 2013, tayari kuuanza Mwaka 2014 kwa baraka na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.