2014-01-01 09:53:49

Jimbo kuu Katoliki Arusha, baada ya Jubilee ya Miaka 50, linajipanga kuadhimisha Sinodi ya pili ya Jimbo!


Askofu mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo kuu Katoliki Arusha katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, baada ya kilele cha Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya uwepo na utendaji wa Jimbo kuu Katoliki Arusha, sasa wanajipanga kusheherekea Sinodi ya Pili ya Jimbo kuu la Arusha, ili kupanga mikakati ya kichungaji na maendeleo kwa Familia ya Mungu, Jimbo kuu Katoliki Arusha. RealAudioMP3

Jubilee ya miaka 2000 ya Ukristo ilikuwa ni chachu ya mikakati ya kichungaji iliyopelekea Maadhimisho ya Sinodi ya kwanza ya Jimbo kuu Katoliki Arusha. Baada ya kilele cha Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya uwepo na utendaji wa Jimbo kuu Katoliki Arusha, sasa Familia ya Mungu inajipanga kupembua mafanikio, mapungufu na changamoto zilizojitokeza katika kipindi cha Miaka 50 iliyopita, tayari kutweka hadi kilindini kwa kujiwekea mpango mkakati wa shughuli za kichungaji na maendeleo kwa Miaka 10 ijayo!

Askofu mkuu Lebulu anasema, dhana ya Familia ya Mungu itaendelea kupewa kipaumbele cha kwanza, kwani hapa kila Mwana familia anahamasishwa kushiriki kikamilifu katika ustawi na maendeleo ya Jimbo kuu Katoliki la Arusha, ili kujenga na kuimarisha sura ya Kanisa la Kristo. Roho Mtakatifu ataendelea kusaidia juhudi na mikakati hii kwani Familia ya Mungu Jimbo kuu Katoliki Arusha inatambua kwamba, wao ni sawa na vyombo vya udongo lakini wanahifadhi hazina kubwa ambayo ni Kristo mwenyewe, anayepaswa kupendwa, kuheshimiwa, kutukuzwa na kutangazwa kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili!

Kilele cha Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya uwepo na utendaji wa Jimbo kuu Katoliki Arusha, kilikuwa ni hapo tarehe 29 Desemba, 2013 wakati Kanisa lilipokuwa linaadhimisha Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Ibada iliongozwa na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam na mahubiri kutolewa na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza. Ibada hii imehudhuriwa na Maaskofu 17 na Mapadri zaidi ya 80 pamoja na umati mkubwa wa watawa na waamini walei!

Katika salam zake, Askofu mkuu Francisco Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, alikazia kwa namna ya pekee udugu kama msingi na njia ya amani unaopaswa kupata chimbuko lake kutoka ndani ya Kanisa. Anasema, siasa na mikakati ya kiuchumi visiishie kwenye teknolojia na kutelekeza tunu na hatima ya kazi ya binadamu; mambo ambayo yanaweza kusababisha chuki na husuda miongoni mwa wananchi bali sera na mikakati ya kiuchumi iwe ni kikolezo cha upendo na mshikamano wa kidugu kati ya wananchi wa Tanzania.

Askofu mkuu Padilla amekazia pia umoja, udugu na mshikamano wa kitaifa, ili kujenga na kuimarisha misingi ya haki, amani na upatanisho. Watanzania waendelee kushikamana kama ndugu, kwa kuheshimu na kuthamini mawazo ya jirani zao; kwa kusaidiana na kusameheana ili kudumisha udugu na amani ambavyo watanzania wamekuwa wakijivunia kwa miaka mingi!

Naye Askofu Oral Sosy wa Kanisa la TAG, Arusha ambaye ni Katibu wa Umoja wa Madhehebu ya Kikristo Mkoani Arusha katika salam zake kwa Jimbo kuu la Arusha anasema, Umoja wao una kazi kuu tau: kuhubiri amani, kuombea Serikali na Nchi ya Tanzania kwa ujumla sanjari na kuangalia masuala ya kijamii.

Umoja huu unaendelea kufuatilia kwa umakini mkubwa mchakato wa Katiba Mpya ya Tanzania. Mambo ambayo wasingependa kuona yanawagawa na kuachanganya watanzania ni: ndoa za watu wajinsia moja, utamaduni wa kifo na masuala ya dini au madhehebu kuingizwa kwenye Katiba ambayo kimsingi ni Sheria Mama.

Kwa upande wake, Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amepongeza Umoja wa Madhehebu ya Kikristo mkoani Arusha kwa kujikita katika: udugu, amani na mshikamano miongoni mwa waamini. Waziri mkuu ambaye alikuwa anamwakilisha rais Jakaya Kikwete wa Tanzania amelipongeza Jimbo kuu Katoliki la Arusha kwa kuasisi Umoja wa Wakristo, mfano wa kuigwa na Mikoa mingine nchini Tanzania. Viongozi wa kidini wasaidie kujenga uchaji wa Mungu miongoni mwa waamini wao, kwani huu ni msaada mkubwa kwa Serikali katika kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani.







All the contents on this site are copyrighted ©.