Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu; Siku ya 47 ya Kuombea amani duniani kwa Mwaka
2014
Mpendwa, unayeitegea sikio Radio Vatican, leo Mama Kanisa anasherehekea sherehe ya
Mama wa Mungu ambayo huja daima kila tarehe mosi ya mwezi Januari.
Ni sherehe
ya amani kwa maana Mama Maria ni Mama wa amani. Amemzaa Mkombozi mfalme wa amani na
hivi Mama Kanisa anaona ni vema tukasali tukimwomba Mungu kwa njia ya Mama huyu kwa
ajili ya amani ya ulimwengu. Sherehe hii ya amani iliwekwa rasmi na Papa Paulo VI
mnamo mwaka 1968.
Salaam Mama Mtakatifu wa Mungu uliyemzaa mfalme mwenye kutawala
mbingu na dunia daima na milele. Hii ndiyo salaam yetu kwa mama mpendelevu, mama asiye
na doa, katika sherehe hii tukufu tunapofungua mwaka mpya. Amani ni tunda ambalo latupasa
kulipalilia daima katika maisha yetu na hivi katika somo la kwanza toka kitabu cha
Hesabu mwandishi anatufundisha namna ya kutunza amani hasa katika wajibu wetu wa kupokea
baraka zitolewazo na Mungu mwenyewe na hasa kwa njia ya Kanisa. Si hilo tu bali hata
wajibu wetu sote kuwabariki na kuwaombea wengine. Wajibu huu kwa namna ya pekee wamekabidhiwa
wazazi katika familia.
Baba na mama wasisahau wajibu huu nyeti wa kubariki
watoto na kuingiza dhana ya baraka katika makuzi ya watoto wao. Ni kwa njia ya makuzi
na malezi, watoto wataweza kuomba baraka kutoka kwa Mungu na kwa Kanisa. Mama Bikira
Maria ni mama mfano mwema ambaye ametenda yote ili Mwanae akue katika hekima na maarifa
kwa ajili ya kutimiza mapenzi ya Mungu.
Mtume Paulo anapowaandikia Wagalatia
anawakumbusha kuwa Kristu amezaliwa chini ya sheria ili aweze kuwakomboa waliochini
ya sheria na hivi kutii mamlaka kwanza na baadaye kuishinda kwa upendo. Utii ni amani
ambayo leo tunaiomba katika sherehe ya Mama wa Mungu.
Somo la injili ni mwendelezo
wa Injili ya usiku wa Noeli. Tunaona wachungaji “kiwakilishi cha waliomaskini” wakiwa
wamezunguka pango wakimsujudia Bwana, ambaye anatunzwa na Maria na Yosefu. Pale hawaoni
alama yoyote ya utukufu bali wanamwona Mkombozi masiha katika nguo za kawaida. Alama
hii yatudai kuwa na imani thabiti ambayo haikai katika kuona bali katika kusikiliza
mwaliko wa Mungu moyoni. Wachungaji walipokwisha kumaliza kazi yao ya kumsujudia Bwana
walirudi katika sehemu yao wakimtukuza Mungu na kusimulia habari hiyo ya furaha.
Yote
haya yalipokuwa yanatendeka Bikira mama mnyenyekevu alikuwa akiangalia na mwisho tunaambiwa
akayaweka yote moyoni”. Jambo hili maana yake ni nini? Ni kwamba Mama Maria anamwona
Mungu katika yote yanayotokea. Ni tofauti nasi ambao wakati fulani tunataka kumwona
Mungu kadiri ya vionjo vyetu, na hata wakati fulani asipoonekana tunakata tamaa.
Kumbe
leo, tujifunze kuyaweka yote moyoni kama Maria Mama wa Mungu. Kwa akina mama wote
Mama Maria ni mfano wa mama mtulivu na mwenye subira iliyojaa hekima ya Mungu, anayetunza
familia takatifu. Kumbe, igeni mfano wake daima kwa ajili ya mafaa ya familia na taifa
la Mungu kwa ujumla.
Ninakutakieni sherehe njema ya Mama Bikira Maria na mwanzo
mwema wa mwaka 2014. Ninatakieni heri Parokia zote zilizowekwa chini ya ulinzi wa
Bikira Maria mama wa Mungu.
Tumsifu Yesu Kristo na Bikira Maria Mama wa Mungu.
Tafakari
hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.