2013-12-31 11:40:24

Hamwezi kufumbia macho madonda ya watu wanaoendelea kuteseka!


Wananchi wa Argentina, tarehe 30 Desemba 2013 wamefanya kumbu kumbu ya miaka tisa tangu Ukumbi wa Muziki wa Pop, uliojulikana kama "Cromanon" ulipowaka moto, na hivyo kupelekea vijana 194 kupoteza maisha.

Baba Mtakatifu Francisko, ametuma ujumbe wa imani na matumaini kwa Askofu Jorge Lozano, rais wa Tume ya Kichungaji ya Baraza la Maaskofu nchini Argentina, akimwomba awafikishie wote walioguswa na janga hili uwepo wake wa karibu. Haya ni madonda ambayo yanaendelea kusababisha machungu katika maisha ya watu, lakini mbaya zaidi, ikiwa kama madonda hao hayashughulikiwi kikamilifu.

Baba Mtakatifu anasema, anapomwangalia Mtoto Yesu, katika hali ya utulivu, anawaombea utulivu huu, ili waweze kutibu madonda haya kwa unyenyekevu mkubwa. Ni madonda ambayo yapo na kamwe watu hawawezi kuyafumbia macho. Ni kwa njia ya ukarimu, ukimya na heshima watu wanaweza kupata faraja.

Anawaombea huruma na upendo kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwafariji kila mmoja wao na kuwafundisha kuonesha mshikamano na ndugu yake. Baba Mtakatifu anawatakia wote Noeli njema.







All the contents on this site are copyrighted ©.