Maandalizi ya Siku ya Familia Kimataifa kwa Mwaka 2015 yanaendelea kupamba moto!
Familia ya Mungu Jimbo kuu la Philadelphia nchini Marekani inaendelea na maandalizi
kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani, itakayoadhimishwa nchini Marekani,
mwezi Septemba 2015. Hili ni tukio
ambalo Kanisa mahalia linashirikiana kwa karibu zaidi na Baraza la Kipapa la familia
ili kuhakikisha kwamba, mambo yanakwenda sawia. Jimbo kuu la Philadelphia limewateuwa
Bibi Donna Farrel na Bwana Jack O’Brien kuwa wakurugenzi waku katika Maadhimisho ya
Siku ya Familia Duniani kwa Mwaka 2015. Askofu mkuu Charles Chaput wa Jimbo kuu
la Philadelphia anasema, kwa sasa wanasubiri kupata ratiba kamili ya Baba Mtakatifu
Francisko katika Maadhimisho haya na kwamba, hili linatarajiwa kuwa ni tukio la aina
yake kwa maisha na utume wa Jimbo kuu la Philadelphia na Marekani katika ujumla wake.
Hii inatokana na ukweli kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kujihusisha na watu
wa kawaida pasi na makuu. Maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani ni Jukwaa muafaka
ambalo litamwezesha Baba Mtakatifu kujisikia kweli yuko nyumbani, ili kushirikiana
nao katika kutangaza Injili ya Furaha pamoja na kuendelea kupambana na kinzani na
vizingiti vya tunu msingi za maisha ya kifamilia kwa ujasiri mkuu pasi na kukata wala
kukatishwa tamaa. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia,
ndoa na familia ni taasisi zinazokabiliana na changamoto nyingi mintarafu mambo ya
maadili na utu wema; sheria na changamoto za kiuchumi na kijamii. Maana ya ndoa
inaanza kuwa ni tungo tata kwa maana kwamba, maana yake ya asili inaanza kumeng’enyuliwa
na kuondolewa katika mpango wa Mungu katika kumshirikisha mwanadamu kwenye kazi ya
Uumbaji. Ndoa sasa inakuwa ni mahali pa kutaka ”kujifurahisha na kujirusha” pasi na
maadili wala dhamana! Askofu mkuu Chaput anasema, Baba Mtakatifu Francisko kwa
kutambua umuhimu, fursa, changamoto na vikwazo vinavyowakabili wanandoa, ameamua kuitisha
Sinodi maalum kwa ajili ya Familia, itakayofanyika mjini Vatican mwezi Oktoba, 2014.
Utakuwa ni muda muafaka kwa Kanisa kutafakari tena juu ya Mafundisho ya Ndoa na Familia
na jinsi ya kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha na utume wa Kanisa. Ni nafasi
ya kupembua kwa kina ni mafundisho yepi ambayo yanakabiliana na kinzani kutoka katika
Jamii na sababu zake. Mababa wa Sinodi watatakiwa kuibua mbinu mkakati wa kuhakikisha
kwamba, Mafundisho haya yanaeleweka vyema zaidi. Maadhimisho haya ni awamu ya kwanza
itakayoweka msingi wa Maadhimisho ya Awamu ya Pili yatakayofanyika kunako Mwaka 2015.
Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume Injili ya Furaha anakazia umuhimu
wa umoja na mshikamano wa Maaskofu katika maisha na utume wa Kanisa, pengine huu utakuwa
ni mwanzo wa utekelezaji wa dira na mwelekeo huu mpya, changamoto kutoka kwa Mababa
wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na ushauri uliotolewa na Makardinali wakati wa
mikutano elekezi kabla ya uchaguzi wa Baba Mtakatifu Francisko. Baraza la Kipapa
la Familia limekwisha watumia Maaskofu mahalia hati ya mwongozo wa Sinodi inayofanyiwa
kazi kwa sasa ili hatimaye, Sekretarieti ya Maaskofu iweze kuyachambua na kutoa hati
ya kutendea kazi, yaani ”Instrumentum Laboris”. Ni mwongozo unaogusia: maana, asili
ya ndoa na familia; changamoto zilizoko. Maaskofu wanaalikwa kujibu maswali dodoso
kwa kuwashirikisha waamini wao. Majibu haya yatasaidia kukoleza majadiliano wakati
wa Sinodi maalum ya Familia itakayofanyika Oktoba 2014. Mchakato huu wa kukusanya
maoni si kura ya maoni kwa ajili ya kutengua Mafundisho Tanzu ya Kanisa, bali ni nyenzo
muhimu inayotaka kulisaidia Kanisa kuona fursa, vikwazo na changamoto katika maisha
ya ndoa na familia. Ni maswali ambayo yamerahisishwa ili kuwawezesha waamini kuyajibu
kwa ufasaha bila kupotosha maana iliyokusudiwa na Baraza la Kipapa la Familia. Askofu
mkuu Charles Chaput anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kumkumbuka
Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na sala zao hasa wakati huu anapojadili masuala
tete katika maisha na utume wa Kanisa.