2013-12-30 10:25:25

Familia ina dhamana kubwa kwa Kanisa na Jamii, ingawa inakabiliwa na changamoto nyingi!


Maadhimisho ya Siku kuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni kielelezo cha upendo mkuu ambao Mwenyezi Mungu amemwonesha mwanadamu kwa kutaka Mwanaye wa Pekee, Yesu Kristo azaliwe katika familia ya binadamu, akiwa na Baba na Mama kama binadamu mwingine yoyote yule!

Liturujia ya Neno la Mungu inaonesha jinsi ambavyo Familia Takatifu ilivyoteseka hadi kukimbilia uhamishoni Misri ili kuokoa maisha ya Mtoto Yesu. Hii ndiyo hali halisi ambayo familia nyingi za wakimbizi na wahamiaji wanakumbana nayo! Hawa ni watu wanaokimbia baa la njaa, vita pamoja na kinzani za kijamii. Ni watu wanaotafuta usalama na maisha bora zaidi kwa ajili yao binafsi na familia zao. Hili ni kundi la watu ambalo wakati mwingine halipokelewi, haliheshimiwi wala kuthaminiwa kutokana na tunu msingi wanazobeba ndani mwao!

Ni watu wanaokabiliana na hali ngumu ya maisha. Familia Takatifu, ivute hisia kwa ajili ya mahangaiko ya wahamiaji na wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za dunia; watu ambao wanakataliwa, wananyonywa na kugeuzwa kuwa ni wahanga wa biashara haramu ya binadamu na utumwa wa nguvu kazi.

Ni tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili iliyopita, wakati Kanisa lilipokuwa linaadhimisha Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Josefu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu amegusia hali ya watu wanaoishi “uhamishoni”, hata pengine bila ya kuonekana. Huu ni uhamisho ndani ya familia yenyewe; hawa ni wazee na watoto wanaonyanyaswa na kuteswa na familia zao!

Baba Mtakatifu anasema, Yesu alipenda kuwa ni sehemu ya Familia kwa kuonja magumu yanayoziandama familia, ili kwamba, asiwepo tena mtu yeyote anayetengwa na uwepo wa Mungu katika maisha yake. Familia Takatifu ililazimika kukimbilia Misri ili kuokoa maisha ya Mtoto Yesu aliyekuwa anawindwa na Mfalme Herode. Hii inaonesha kwamba, Mwenyezi Mungu yupo pale ambapo mwanadamu anapokataliwa na kutengwa; Mungu pia yupo pale mwanadamu anapoota ndoto na kuwa na matumaini ya kuweza kurudi kwa uhuru kamili katika nchi yake mwenyewe; pale anapopanga na kuamua kuhusu maisha na utu wake mwenyewe na familia yake kwa ujumla.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kujenga na kudumisha familia ambazo zitakuwa ni: Jumuiya za upendo, ukarimu na upatanisho; daima zikijitahidi kusaidiana na kusameheana, ili kujenga na kuimarisha: amani na furaha ya kweli katika familia. Amewataka wanafamilia kujikita katika maneno makuu matatu msingi katika maisha ya kifamilia: Samahani, Asante, Nisamehe.

Wanafamilia watambue umuhimu wao katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Utangazaji wa Injili unapata chimbuko lake katika familia na baadaye, kuenea katika hatua mbali mbali za maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu anawahimiza wanafamilia wote kutekelea utume waliokabidhiwa na Mwenyezi Mungu kwa heshima na utulivu.

Baba Mtakatifu wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, alikuwa ameunganishwa kwa njia ya video na waamini waliokuwa wamekutanika mjini Nazareti, Barcelona na Loreto kwa ajili ya kuombea Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia, itakayoadhimishwa, Mwezi Oktoba, 2014.








All the contents on this site are copyrighted ©.