2013-12-30 14:49:32

Askofu Nunzio Galantino ateuliwa kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia


Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 28 Desemba 2013 amemteua Askofu Nunzio Galantino kutoka Jimbo Katoliki la Cassano all'Jonio, Italia kuwa Katibu mkuu wa muda wa Baraza Maaskofu Katoliki Italia.

Akizungumzia kuhusu uteuzi huu, Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Askofu Galantino ameteuliwa kuwa Katibu mkuu kwa muda usiojulikana na ataendelea kutekeleza utume wake kama Askofu wa Jimbo Katoliki Cassano. Lengo ni kuendeleza shughuli za Baraza la Maaskofu Katoliki Italia na kwamba, muda mrefu itambidi kuwa mjini Roma.

Baba Mtakatifu Francisko ameandika barua kwa Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Cassano all'Jonio, Italia akiwatakia kheri na baraka wakati huu wa kipindi cha Noeli na Mwaka mpya 2014. Anasema, anatarajia siku moja, kuonana nao, ili waweze kufahamiana zaidi.

Kwa namna ya pekee, anawaomba, waamini wa Jimbo hili kumruhusu Askofu Galantino kutekeleza dhamana yake kama Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Anatambua usumbufu watakaokutana nao kwa vile wanampenda sana Askofu wao, lakini anawaomba wamsamehe na kumruhusu Askofu Galantino afanye utume huu mpya ambao ni sadaka kubwa, kwani itambidi asafiri mara kwa mara na kwamba, anahitaji msaada wa sala zao katika hija hii ya imani!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufahamu kuhusu uteuzi huu na kuendelea kumwombea katika maisha na utuke wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.







All the contents on this site are copyrighted ©.