2013-12-28 08:53:20

Yaliyojiri Jimboni Dodoma, Siku kuu ya Utoto Mtakatifu!


Watoto 1,500 kutoka Parokia mbali mbali za Jimbo Katoliki Dodoma, Ijumaa tarehe 27 Desemba 2013 wameshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufanya kumbu kumbu ya Watoto mashahidi waliouwawa kikatili na Mfalme Herode, kutokana na wasi wasi wa kudhani kwamba, Mtoto Yesu alikuwa anakuja kumpora madaraka yake!

Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika kwenye Parokia ya Mtakatifu Gaspar del Buffalo, Makole, imeongozwa na Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma. Watoto wametakiwa kuonesha moyo wa shukrani kwa wazazi na walezi wao, bila kusahau kuwa na ibada pamoja na uchaji kwa Mwenyezi Mungu anayewakirimia neema na baraka katika hija ya maisha yao hapa duniani. Mungu ni Baba mwenyezi anayawaongoza watoto wake katika njia ya amani, haki na utakatifu.

Askofu Nyaisonga katika mahubiri yake, amewataka watoto kuonesha moyo wa shukrani kwa wazazi na walezi wao kutokana na: tunza na malezi bora wanayowakirimia; ikiwa ni pamoja na elimu, afya pamoja na mahitaji yao msingi, bila kusahau kwamba, imani waliyonayo ni urithi mkubwa kutoka kwa wazazi wao, changamoto ya kuilinda, kuikuza na kuendeleza.

Mtoto Yesu alipozaliwa, amri ilitoka kwa Mfalme Herode aliyekuwa amesikia habari kutoka kwa Mamajusi kuhusu kuzaliwa kwa Mfalme wa Wayahudi, jambo ambalo lilimhuzunisha sana, kiasi cha kuingiwa na hofu pamoja na wasi wasi mkubwa. Matokeo yake akaamuru watoto wote waliokuwa na umri chini ya miaka miwili wauwawe. Lakini kwa maongozi na tunza ya Mwenyezi Mungu, Mtoto Yesu aliweza kuokolewa na Mtakatifu Yosefu na Bikira Maria waliokimbilia ugenini nchini Misri.

Askofu Nyaisonga anasema, hata baada ya miaka zaidi ya elfu mbili kupita, bado kuna akina Herode wanaoendelea kujitokeza duniani kwa kukumbatia utamaduni wa kifo unaosimikwa katika sera za utoaji mimba, ubinafsi, uchoyo na mmong'nyoko wa maadili na utu wema. Kuna maelfu ya watoto wanaopoteza maisha yao sehemu mbali mbali za dunia kwa kutolewa mimba; kuna kundi kubwa la watoto linaloishi katika mazingira hatarishi na kwamba, kuna watoto ambao wamekata tamaa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Watoto wote hawa wamekumbukwa katika sala na sadaka iliyotolewa kwa ajili yao!

Askofu Nyaisonga amewataka watoto waliobahatika kupata urithi wa imani na matunzo bora ya kifamilia, kusimama kidete kulinda na kutetea imani yao na kamwe wasikubali kuyumbishwa na watu wanaofanana na akina Herode, waliomezwa na ubinafsi kiasi cha kutaka kukatisha maisha ya watoto kinyume cha mpango na mapenzi ya Mungu. Wazazi na walezi wajenge tabia ya kuwapenda, kuwaheshimu na kuwathamini watoto! Wawasaidie kukuza karama na vipaji vyao; wawe mstari wa mbele kuwapatia mahitaji yao msingi pamoja na kuhakikisha kwamba, haki msingi za watoto zinalindwa na kuheshimiwa.

Katika Ibada hii ya Misa Takatifu, Watoto 119 waliimarishwa katika Ukristo wao kwa kupewa Sakramenti ya Kipaimara inayokuza na kuzamisha zaidi neema ya Sakramenti ya Ubatizo: kwa kufanyika waana wa Mungu na ndugu zake Kristo; kwa kupokea mapaji ya Roho Mtakatifu na kuunganishwa zaidi na Kanisa. Sakramenti ya Kipaimara inawapatia waamini nguvu ya pekee kutoka kwa Roho Mtakatifu kwa ajili ya kueneza na kutetea Imani kwa maneno na matendo kama Mashahidi wa kweli wa Kristo bila kuuonea aibu Msalaba wa Kristo. Wakristo hao wamepokea mhuri wa Roho Mtakatifu.

Katika Ibada hii ya Misa Takatifu, Wanachama wapya wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu Jimbo Katoliki Dodoma walipokelewa rasmi na wale wa zamani wamerudia ahadi zao. Makamu Mwenyekiti Baraza la Walei, Jimbo Katoliki Dodoma alikula kiapo cha utii. Maskauti wapya walipata pia fursa ya kula kiapo pamoja na kupandishwa vyeo. Chama cha Skauti ni matunda ya kazi na utume wa Askofu Nyaisonga, Jimbo Katoliki Dodoma, kwa lengo la kutaka kuwashirikisha watoto katika maisha na utume wa Kanisa.

Jimbo Katoliki Dodoma limezindua pia Programme ya Neno la Mungu kwa njia ya kusikiliza, ili kutoa fursa kwa waamini, vikundi na watu wenye mapenzi mema kusikiliza Neno la Mungu kwa njia ya kisasa. Hii ni Programe iliyoandaliwa na Chama cha Biblia Mkoa wa Dodoma, chini ya Mwenyekiti wake mpya Askofu Bernardine Mfumbusa wa Jimbo Katoliki Kondoa.

Na Rodrick Minja,
Kutoka Dodoma.







All the contents on this site are copyrighted ©.