2013-12-28 07:55:07

Watoto mashahidi waliouwawa kikatili enzi ya Mfalme Herode


Mashahidi na wafiadini wanatoa ushuhuda kwa Kristo na Kanisa lake si tu kwa njia ya maneno, bali kwa kuyamimina maisha yao. Wafiadini na mashahidi wanaendelea kulikumbusha Kanisa kwamba, kifodini ni zawadi kubwa kutoka kwa Yesu Kristo mwenyewe. Tarehe 28 Desemba, kila mwaka, Mama Kanisa anawakumbuka watoto waliouwawa kikatili na Mfalme Herode, alipokuwa anayawinda maisha ya Mtoto Yesu.

Watoto hawa ni kati ya wale wanaomzunguka Mwanakondoo wa Mungu na kwa njia ya ushuhuda makini wa watoto hawa, Mama Kanisa anapenda kukumbusha umuhimu wa kuthamini, kulinda na kutetea ut una heshima ya watoto.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Injili ya Furaha anabainisha kwamba, Uinjilishaji ni dhamana inayotekelezwa na Mama Kanisa kwa kufuata amri ya Kristo, kwenda duniani kote ili kubatiza na kuwafundisha yote aliyo agiza. Dhamana hii inatekelezwa na Familia yote ya Mungu katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kichungaji, Dhamana ya Afrika anasema kwamba, watoto ni zawadi ya Mungu kwa wanadamu, kumbe, wanapaswa kuwa ni lengo la: Familia, Kanisa, Serikali na Jamii katika ujumla wake, kwani watoto ni chanzo cha matumaini na maisha mapya. Mwenyezi Mungu yuko karibu na watoto na kwamba, wanathamani kubwa sana mbele yake. Mtoto ana haki ya kuishi na kwamba, Kanisa Barani Afrika lazima lisimame kidete kuwalinda na kuwatetea watoto tangu pale wanapotungwa mimba tumboni mwa mama zao hadi mauti ya kawaida inapowafika.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI anaendelea kusema kwamba, ni jukumu la Kanisa kuhakikisha kwamba, linaruhusu mwanga wa Kristo ung’ae maisha ya watoto kwa kuwapatia upendo wake kwani kwa hakika wana thamani kubwa sana mbele yake. Mwenyezi Mungu anataka kila mtoto awe na furaha na tabasamu; na upendeleo wake uwe juu yao, kwani ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu wanyenyekevu kama walivyo watoto.

Tarehe 28 Desemba ya kila Mwaka, Mama Kanisa anafanya kumbu kumbu ya Watoto waliouwawa kikatiliki na Mfalme Herode alipokuwa anamtafuta Mtoto Yesu aliyekuwa amesikia habari zake. Hii ni Siku ambayo Shirika la Utoto Mtakatifu nchini Tanzania linafunga Mwaka wa Imani rasmi.

Padre Deusdedith Mulokozi, C.PP.S anaangalia msingi wa Utoto Mtakatifu, Majukumu ya wazazi na lengo kuu la Chama cha Utoto Mtakatifu. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kanisa linaendelea kuwekeza katika malezi na makuzi ya Watoto ili waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina kwa watoto wenzao!

I MSINGI WA UTOTO MTAKATIFU

    Ni utoto mtakatifu wa Yesu
    Ni mwaliko wa Mkombozi wetu Yesu Kristo
    Waache watoto waje kwangu kwa maana ufalme wa Mungu ni wao (Mt. 19:14)
    Anawaita wawe rafiki, wasaidizi na wamisionari wake kwa yale mengi aliyowatendea
    Wanaitwa waishi ujumbe wanaoitwa kuupeleka kwanza kabla ya kuupeleka kwa wengine\ujumbe huo ni Injili Takatifu yaani habari njema kwetu sisi sote
    Yesu hana mikono, macho, mdomo, miguu au nguo ya kuvaa, kwa sasa yeye ni maskini wa maskini, na hivyo anataka mtumie mikono, macho, midomo na yote mliyo nayo kusaidia maskini
    Nilikuwa na njaa mkanipa chakula, nilikuwa na kiu mkanipa maji, nilikuwa uchi mkanivika, nilikuwa mgonjwa mkaja kunitazama, nilikuwa gerezani mkaja kunitembelea (Mt. 25:34-37).
    Watoto wa Utoto Mtakatifu, wanaalikwa kuwa watu wa IBADA, KUSHIRIKI SAKRAMENTI ZA KANISA NA HASA KITUBIO NA MISA TAKATIFU

II MAJUKUMU YA WAZAZI

    Wazazi tunzeni uhai, ninyi ndio wamisionari wa kwanza tangu dakika ya uhai wa mwanadamu
    Mfunze mtoto namna ya kuishi vizuri naye hatasahau njia hiyo hata uzeeni (Methali 22:6)
    Wazazi wawe alama ya furaha katika familia na uhai wa kanisa
    Mwache Roho Mtakatifu afanye miujiza yake kwa ninyi kujifungua mioyo yenu

III LENGO
    Watoto wasaidie watoto wenzao
    Kufikia lengo hilo inawapasa wazazi, walezi, makatekista, walimu wa dini, watawa, mapadre kuwapa malezi bora ya Imani Katoliki
    Kuwasaidia kujua utume wao
    Yesu anapenda watoto waokolewe kutoka kila aina ya uovu kimwili na kiroho
    Kumtafutia Yesu marafiki wa Imani yao na wasio wa imani yao.


Fadre Mulokozi Deusdedit, C.PP.S.







All the contents on this site are copyrighted ©.