Wanajeshi 5,500 wa Umoja wa Mataifa wapelekwa kulinda raia na mali zao
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeamua kwa akuli moja kuongeza idadi ya wanajeshi
wa kulinda amani nchini Sudan ya Kusini ambayo kwa sasa iko kwenye vita ya wenyewe
kwa wenyewe.
Taarifa ya Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon
inaonesha kwamba, wanajeshi 5, 500 kutoka Umoja wa Mataifa wanapelekwa Sudan ya Kusini
ili kuongeza nguvu katika mchakato wa kulinda raia na mali zao. Umoja wa Mataifa unasema
kwamba, kuna zaidi ya watu laki moja moja ambao kwa sasa wanaishi kwenye Kambi maalum
za wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi nchini Sudan ya Kusini.
Kuna idadi
kubwa ya raia ambao wamepoteza maisha yao kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe
inayoendelea Nchi Sudan. Hata hivyo juhudi za Jumuiya ya Kimataifa ya kutaka kupata
suluhu ya amani na utulivu zinaendelea kufanyika ndani na nje ya Sudan ya Kusini.
Wanachama wa IGAD chini ya Rais Yoweri Museveni wa Uganda wanafuatilia kwa karibu
zaidi machafuko ya kisiasa nchini Sudan ya Kusini kwani athari zake ni kubwa pia hata
kwa nchi majirani.