Hija ya kiroho katika mazingira ya Yesu kwenye Nchi Takatifu
Mahujaji 55 kutoka Tanzania wanaotembelea Nchi Takatifu kama sehemu ya mchakato wa
kukuza na kuimarisha imani, tayari kuitolea ushuhuda katika maisha wanasema, hija
hii ya maisha ya kiroho imekuwa na mafanikio makubwa katika maisha yao. Wamepata nafasi
ya kusali mahali alipozaliwa Yesu Kristo Mkombozi wa dunia pamoja na kutembelea maeneo
matakatifu Mjini Yerusalem.
Mahujaji hao wamekwenda hadi Bethania, nyumbani
kwao Martha na Maria; wakaona kaburi la Lazaro. Wanasema, hapa wamekumbushwa umuhimu
wa sala na kazi, kama ambavyo Yesu mwenyewe alifafanua alipokuwa anazungumza na Maria
aliyekuwa amechagua fungu bora zaidi sanjari na kujenga urafiki wa dhati na Yesu,
hali ambayo ilimfanya hata Yesu kumlilia rafiki yake Lazaro. Watu waguswe na majanga
ya jirani zao na hivyo kuepukana na utandawazi usiojali wala kuguswa na shida za wengine
kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko.
Mahujaji hao wa Tanzania wamepata
fursa ya kutembelea mjini Yeriko; wakapanda Mlimani ambako Yesu baada ya kufunga kwa
siku arobaini mchana na usiku bila kula, alishawishiwa na Ibilisi, lakini akashinda
mitego yote ya Ibilisi. Waamini wanakumbushwa umuhimu wa kusali na kufunga kama njia
ya kudhibiti vilema na mapungufu yao ya kibinadamu.
Mahujaji wametembelea
Bahari ya Sham, wakakumbushwa umuhimu wa Sakramenti ya Ubatizo na jinsi Waisraeli
walivyookolewa kutoka utumwani Misri kwa mkono wa nguvu na maajabu kutoka kwa Mwenyezi
Mungu. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanatumwa kuwa ni Manabii, Wafalme na Makuhani
katika Familia, Jumuiya na Mahali pao pa kazi, tayari kumshuhudia Kristo na Kanisa
lake kwa njia ya maisha adili.
Mahujaji hawa katika mahojiano maalum na Radio
Vatican wanasema wamevutiwa sana na mapango ya Jumuiya ya Qumran, mahali ambapo wataalam
waligundua Maandiko Matakatifu yaliyokuwa yamehifadhiwa kwenye Mapango. Wamekumbushwa
umuhimu wa kusoma, kutafakari na kumwilisha utajiri wa Neno la Mungu katika maisha
yao ya kila siku! Wanasema, eneo hili ni Jangwa sana, kiasi cha kushindwa kutambua
ile ahadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuhusu "asali na maziwa".
Kwa hakika,
hija hii ya maisha ya kiroho, imekuwa ni kikolezo kikubwa cha imani katika matendo;
kwa sasa wana upeo na ufahamu mkubwa kuhusu mazingira ya Yesu na Maandiko Mtakatifu
kwa ujumla wake! Waisraeli ni watu wanaoishi katika mazingira magumu, lakini Mwenyezi
Mungu amewajalia kipaji cha akili na ugunduzi, kiasi kwamba, daima wanajitahidi kuendeleza
ile kazi ya uumbaji, laiti kama amani, utulivu vingekuwepo, bila shaka Waisraeli leo
hii wangekuwa mbali katika maendeleo! Ni mshangao wa baadhi ya mahujaji kutoka Tanzania
huko Nchi Takatifu!
Mahujaji 55 kutoka Tanzania wanajiandaa kwenda Galilaya,
huko ambako Yesu alitumia muda wake mwingi kuhubiri; hapa wanatarajia kula samaki
na wanandoa watano wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Familia Takatifu ya Yesu,
Maria na Yosefu, watarudia tena ahadi zao za Ndoa, tayari kumshuhudia Kristo na Kanisa
lake kwa maisha ya kifamilia kadiri ya mpango wa Mungu.