Jubilee ya Miaka 50 Jimbo kuu la Arusha: Changamoto ni hofu na vizingiti vya mila
na tamaduni... Lakini! Angalia na ushangae mwenyewe!
Waswahili wana mambo! Eti penye msafara wa Mamba, hapo hapo Kenge hakosi! Leo katika
mahojiano maalum kati ya Radio Vatican na Askofu mkuu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo
kuu Katoliki Arusha, Tanzania wakati huu wanapojiandaa kwa kilele cha Maadhimisho
ya Jubilee ya Miaka 50 ya Uwepo na Utendaji wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha, anazungumzia
changamoto kuu mbili: hofu na utamadunisho!
Askofu mkuu
Lebulu anasema kwamba, pale ambapo Yesu anachapa kazi yake barabara, hapo kwa hakika
Shetani hawezi kukosekana ili kuvuruga kazi njema inayofanywa na Yesu kwa njia ya
wafuasi wake. Mlipuko wa bomu uliotokea wakati wa kutabaruku Kanisa la Parokia ya
Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, ulikuwa ni mkono wa Iblisi, kutaka kuwaogopesha waamini
wasifurahie na kuzama katika furaha ya ukombozi. Hizi zilikuwa ni jitihada za makusudi
za kufisha ari na mwamko wa imani Jimbo kuu Katoliki la Arusha.
Askofu mkuu
Lebulu anasema, Kanisa lililolipuliwa kwa bomu, kilikuwa ni kielelezo wazi cha Maadhimisho
ya Jubilee ya Miaka 50 ya uwepo na utendaji wa Jimbo kuu Katoliki Arusha. Waamini
walikuwa wamekusanyika kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Imani Katoliki, hapo wakalipuliwa
kwa bomu, ili kuwajengea hofu na mashaka makubwa.
Badala ya waamini kukata
na kukatishwa tamaa na vitendo hivi, badala yake, waamini wameshinda hofu na wasi
wasi; wamepata ari na mwamko mpya, tayari kujitosa kimasomaso kushuhudia imani yao
kwa Kristo na Kanisa lake, bila woga wala makunyanzi kwani wanasema, ikiwa kama Kristo
akiwa upande wao! Mwanadamu atawatenda nini? Badala ya kukatishwa tamaa, waamini wameimarishwa
zaidi katika imani!
Askofu mkuu Lebulu anaendelea kusema kwamba, kuna baadhi
ya waamini wanakata tamaa kwa kudhani kwamba, hatua waliyofikia katika imani bado
ni kidogo sana na kwamba, imani kwa kiasi kikubwa bado inayumba na kukutana na vizingiti
katika mila na tamaduni nyingi za waamini wa Jimbo kuu Katoliki la Arusha. Kuna mambo
mengi bado yanasigana na kweli za Kiinjili na kumbe, hii ni changamoto kutoka katika
undani wa maisha ya waamini wenyewe na hii ni kali zaidi kuliko hofu ya kifo!
Askofu
Mkuu Lebulu anasema, inachukua muda mrefu kubadili mila, tamaduni na desturi za watu.
Jimbo kuu Katoliki Arusha, linamwomba Yesu mwenyewe aguse tamaduni zao, ili kuwakomboa,
kwani amekuja kuwakomboa watu na mazingira yao. Bado kuna changamoto ya kuendelea
kutamadunisha Injili, ili kusafisha na kukatasa yale mambo ambayo yanasigana na tunu
msingi za Kiinjili.