Kuanzia tarehe 28 Desemba hadi tarehe Mosi, Januari 2014, Vijana kutoka Bara la Ulaya
watakuwa wanafanya mkutano wa 36 wa Vijana ulioandaliwa na Jumuiya ya Kiekumene ya
Taizè huko Strasburg, Ufaransa. Vijana watakapofika mjini humo watapokelewa na kupewa
hifadhi na familia pamoja na taasisi mbali mbali na baadaye kushiriki katika sala
ya jioni.
Wakati wote
huu, vijana watakuwa wanashiriki katika Ibada za Misa Takatifu kwenye Parokia mbali
mbali na jioni watakuwa wanakusanyika kujadili kuhusu tasahufi ya maisha ya kiroho:
Watagusia pia masuala ya kijamii, kihistoria na kisanaa Barani Ulaya.
Vijana
watakuwa na fursa ya kusali kwa pamoja kwenye Uwanja wa Wacken. Jumatatu tarehe 30
Desemba na Jumanne tarehe 31 Desemba, 2013, Vijana watakuwa na ratiba maalum ya kusali
kwa ajili yakuombea amani duniani pamoja na kuadhimisha Siku kuu ya Wenyeji itakayoenea
sehemu mbali mbali ambazo vijana watakuwa wanaonjeshwa ukarimu na wananchi wa Ufaransa
katika ujumla wao.
Tarehe Mosi, Januari 2014 baada ya kupata chakula cha mchana
kwenye familia na taasisi zinazowakirimia, vijana watakunja virago na kuanza safari
ya kurudi kwenye nchi zao, tayari kumwilisha uzoefu na mang’amuzi ya maisha ya kiroho
waliyofainikiwa kupata katika kipindi hiki.
Baba Mtakatifu Francisko katika
ujumbe wake kwa Vijana wa Jumuiya ya Taizè anawakumbusha juu ya Maadhimisho ya Siku
ya 35 ya Vijana wa Taizè yaliyofanyika mjini Roma kwa kusali pamoja na Baba Mtakatifu
mstaafu Benedikto XVI, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Papa Francisko anasema, kwa hakika Roma wakati ule ilisheheni umati wa vijana kutoka
sehemu mbali mbali za Bara la Ulaya.
Baba Mtakatifu anawaambia vijana hawa
kwamba, anawategemea katika ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; ili kujenga
na kuimarisha moyo wa amani na upatanisho, ili hatimaye, Injili iweze kuota mizizi
yake kwenye mioyo ya vijana wengi Barani Ulaya.
Mheshimiwa Martin Junge, Katibu
mkuu wa Shirikisho la Makanisa ya Kiluteri Duniani anawapongeza vijana kwa kuamua
kushiriki katika tukio hili la kidini linalobubujika furaha ya pekee kwani: vijana
wanapotembea huku wakisali na kuimba, watakuwa wanashiriki katika mchakato wa kujenga
na kudumisha mshikamano mpya. Mheshimiwa Junge anawatakia kila la kheri na baraka
tele katika ujenzi wa dunia mpya inayosimikwa katika haki, amani na mshikamano wa
dhati.
Bwana Ban Ki-Moon, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa katika salam zake
anabainisha kwamba, teknolojia ya mawasiliano imekuwa na kupanuka kiasi cha kuwafanya
watu kujisikia kuwa wa moja. Changamoto iliyoko mbele ya Jumuiya ya Kimataifa ni kujenga
na kuimarisha moyo wa huruma na uraia wa kimataifa. Lengo liwe ni kuunganisha dunia,
huku watu wenyewe wakiwa wameungana. Watu wana malengo tofauti ya maisha, lakini hawana
budi kujenga na kuimarisha ushirikiano mpana zaidi, hii ndiyo mantiki ya utandawazi
kwa sasa.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema kwamba, anawategemea vijana
kumwilisha malengo msingi ya Umoja wa Mataifa katika kukuza na kudumisha misingi ya
amani, maendeleo endelevu na haki msingi za binadamu.
Bwana Herman van Rompuy,
Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya katika ujumbe wake kwa vijana wa Taizè wanakutanika
mjini Strasburg, Ufaransa anawataka vijana kuvuka kizingiti cha utengano; kwa kukazia
upatanisho na umoja miongoni mwa Wakristo ili kujenga Kanisa moja, kadiri ya kauli
mbiu inayoongoza Maadhimisho ya 36 ya Vijana wa Taizè Barani Ulaya.
Kauli
mbiu inakazia pamoja na mambo mengine umoja katika utofauti; na umoja kwa njia ya
neema katika utofauti. Haya ni mambo ambayo Baraza la Ulaya limeendelea kuyafanyia
kazi kama sehemu ya vipaumbele vyake katika ujenzi na maendeleo ya Ulaya.