2013-12-26 09:41:45

Mahujaji kutoka Tanzania wako Yerusalem!


Kikundi cha mahujaji 55 kutoka Tanzania kinachofanya hija ya maisha ya kiroho katika Nchi Takatifu kama sehemu ya mchakato wa kuimarisha na kukoleza imani mara baada ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, wakati wa Sherehe za Noeli, 25 Desemba 2013, wameshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika kwenye Kanisa la Kuzaliwa Bwana mjini Bethlehemu.

Kanisa hili lilipambwa kwa mishumaa iliyokuwa inawaka kielelezo cha Kristo Mwanga wa Mataifa! Watu wamesali kwa imani, matumaini na mapendo makubwa! Ibada imehudhuriwa na umati mkubwa wa mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia! Kwa hakika hawa ni watu wanaofanya hija ya kumtafuta Kristo Mwanga wa Mataifa!

Baadhi ya mahujaji kutoka Tanzania wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wanasema, kwa mara ya kwanza katika historia ya maisha yao ya Kikristo wameonja na kushuhudua imani ya Wakristo inayobubujika kutokana na Fumbo la Umwilisho, linalopata ukamilifu wake kwenye Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Yesu. Mahujaji kutoka Tanzania wanasema, wametembelea Kalvari na Golgota; wamesali na kutafakari historia ya kazi ya ukombozi. Kwa hakika haya ni matendo makuu ya Mungu!

Mahujaji hao kutoka Tanzania wanasema, wanaendelea na hija yao ya maisha ya kiroho kwa kutembelea: Kapernaumu na Kana ya Galilaya, mahali ambapo kwa mara ya kwanza Yesu alifanya muujiza wake wa kwanza hadharani, alipombwa na Bikira Maria kuokoa "Jahazi la wanandoa wapya" waliokuwa wametindikiwa na divai! Mahujaji hawa wanasema, hata katika maisha ya ndoa na familia, kuna wakati mwingine wanandoa wanatindikiwa na divai ya: "uvumilivu, udumifu, maisha ya sala na tafakari; upendo na uaminifu".

Kumbe, kuna haja kila wakati kumkaribisha Yesu na Bikira Maria katika maisha ya kifamilia, ili mambo yote yaweze kuwa supa! Bethlehemu ni mahali ambapo wameonja na kugusa kwa macho yao ya imani: ujumbe wa amani, haki, upendo na upatanisho! Hii ndiyo changamoto inayowakabili Watu wa Mataifa kwa nyakati hizi wanasema mahujaji kutoka Tanzania. Hija ya kiroho Nchi Takatifu na Misri inapania kukoleza imani katika matendo!







All the contents on this site are copyrighted ©.