2013-12-25 09:40:11

Yesu ni Mfalme wa Amani, Hakimu mwenye haki; ni chemchemi ya furaha kwa wengi!


Waamini wanatakiwa kuiga mfano wa Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu, waliokuwa mstari wa mbele katika kutekeleza maagizo halali ya sheria ya sensa ya watu na makazi kwa wakati wao! Na serikali kwa upande wake, inapaswa kuwa na mipango na mikakati madhubuti kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wake katika nyanja mbali mbali za maisha, daima ikilenga kutafuta mafao ya wengi, haki na amani!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma katika kesha la Siku kuu ya Noeli, lililofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimboni Dodoma. Anasema, Mtakatifu Yosefu alikuwa ni mtii kwa Mungu na Serikali. Yesu aliyezaliwa mjini Bethlehemu ni Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele; Mfalme wa Amani na hakimu mwenye haki! Yesu Kristo ni chemchemi ya furaha na amani kwa watu wake, changamoto ya kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki, amani na mshikamano wa kitaifa.

Askofu Nyaisonga anasema kwamba, Mtoto Yesu aliyezaliwa ni mwanga unaowaangazia wale wanaotembea katika giza la dhambi na mauti, changamoto kwa waamini kuanza kuona mwanga na kuufuata, kwani Yesu aliyezaliwa amekuja ulimwenguni ili kumkomboa na kumtakasa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi, ili hatimaye, kuwapatanisha wanadamu na Mungu wao pamoja na binadamu wenzao.

Yesu Kristo amezaliwa katika hali ya umaskini mkubwa, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanajenga na kuimarisha mshikamano wa dhati na wa kidugu na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili wao pia waonje na kufurahia uwepo wa Mungu katika maisha yao. Jamii ya wafugaji ndiyo iliyobahatika kwanza kabisa kusikia Injili ya Furaha ikitangazwa masikioni mwao!

Changamoto kwa Jamii kuheshimu na kuthamini Jamii za kichungaji kwa kuzipatia haki zake msingi na kuepusha migogoro na kinzani ambapo wakati mwingine zimepelekea hali ya kuvunjika kwa amani sehemu mbali mbali za Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Kila mtu anathamani na asili yake mbele ya Mwenyezi Mungu. Waamini washinde kishawishi cha kukata tamaa kwa kujenga matumaini yanayowawezesha kusimama kidete ili kukabiliana na magumu pamoja na vizingiti vya maisha, hadi ufumbuzi upatikane.

Askofu Gervas Nyaisonga amewataka waamini kutekeleza dhamana na majukumu yao barabara, kwa kudumisha, haki, amani, upendo na mshikamano! Kuzaliwa kwa Yesu Kristo Mkombozi wa dunia, kuwainue wanyonge na wadhaifu, kwa kutambua kwamba, wana thamani kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Imeandaliwa na
Rodrick Minja,
Dodoma.







All the contents on this site are copyrighted ©.