2013-12-25 10:58:40

Kanisa linawakumbuka waliotekwa nyara na kupotea katika mazingira ya utatanishi huko Mashariki ya Kati!


Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaendelea kuyahamasisha Makanisa wanachama kusali kwa ajili ya kuombea haki, amani na upatanisho wa kitaifa nchini Syria, ili kwamba, viongozi mbali mbali wa Makanisa waliotekwa nchini humo waweze kurudi na kuendelea na utume wao kwa amani na usalama.

Itakumbukwa kwamba, tangu tarehe 2 Desemba 2013 kuna watawa kumi na wawili walitekwa nyara na watu wasiofahamika na hadi sasa hawajulikani waliko. Kanisa linaadhimisha Noeli, wakati ambapo bado kuna Maaskofu wawili wa Kanisa la Kiorthodox nchini Syria waliotekwa miezi kadhaa iliyopita ambao bado hawajaonekana.

Ni mwaliko kutoka kwa Dr. Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, wakati huu Mama Kanisa anaposherehekea Siku kuu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo Mfalme wa Amani. Kutekwa kwa viongozi hawa wa Makanisa ni jambo ambalo linaendelea kutonesha madonda na machungu wanayokabiliana nayo wananchi wa Syria kutokana na vita, kinzani na migogoro ya kijamii. Kuna watu ambao wamefungwa na hatimaye, kupotea katika mazingira tatanishi.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linawaalika wadau mbali mbali wa mgogoro wa kivita nchini Syria, kutekeleza wajibu wao kwa ajili ya mafao na ustawi wa maendeleo ya wananchi wa Syria katika ujumla wake. Viongozi wa kidini wasitumiwe kama ngao bali wawe ni kikolezo cha mshikamano wa upendo na upatanisho wa kitaifa na wala si vinginevyo. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusaidia harakati za kudhibiti vitendo vya utekaji nyara wa watu wasiokuwa na hatia.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaendelea kuyahamasisha Makanisa wanachama na watu wote wenye mapenzi mema, kusali kwa ajili yakuombea amani na mshikamano wa kitaifa nchini Syria. Wanaungana na wote wanaoomboleza kutokana na kuondokewa na ndugu na jamaa zao katika mazingira ya utatanishi. Dr. Tveit anasema, uwepo wa Wakristo huko Mashariki ya Kati, uwe ni ushuhuda wa imani hata katika hali ngumu ya maisha!







All the contents on this site are copyrighted ©.