2013-12-25 09:02:24

Jubilee ya Miaka 50 ya uwepo na utendaji wa Jimbo kuu Katoliki Arusha!


Jimbo kuu Katoliki la Arusha, Tanzania liko kwenye pilika pilika za Maadhimisho ya Jubilee ya Dhahabu ya uwepo na utendaji wake na kilele cha Maadhimisho haya ni hapo tarehe 29 Desemba 2013, Familia ya Mungu Jimbo kuu la Arusha itakapomwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani, likiendelea kuomba tunza na neema katika maisha na utume wake! RealAudioMP3

Hii itakuwa ni Siku kuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Ibada ya Misa Takatifu inatarajiwa kuadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu.

Askofu mkuu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu Arusha katika mahojiano maalum na Radio Vatican anapembua kwa kina na mapana mafanikio yaliyopatikana tangu Jimbo kuu la Arusha lilipoanzishwa kunako mwaka 1963, si kwa ajili ya kujivuna, bali ni kumtolea Mwenyezi Mungu sifa na shukrani kwa ukarimu wake kwa waamini wa Jimbo kuu la Arusha.

Anazungumzia kuhusu changamoto wanazokabiliana nazo, si kwa ajili ya kukata wala kujikatia tamaa, bali kuona vikwazo na vizingiti katika maisha na utume wa Kanisa Jimbo kuu la Arusha, tayari kuvivalia njuga, ili kupambana navyo hadi kieleweke, yaani kwa kukazia Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Askofu mkuu Lebulu anafafanua baadhi ya mambo ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi baada ya Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya uwepo na utendaji wa Jimbo kuu Katoliki la Arusha. Anasema, Kipindi kuanzia mwaka 1963 hadi mwaka 2013, kimekuwa ni kipindi cha neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Uwepo na utendaji wa Jimbo kuu Katoliki Arusha, sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, imekuwa ni fursa ya Uinjilishaji wa kina, wazo msingi ni kutaka kuhakikisha kwamba, Injili inagusa: mioyo, akili na maisha ya watu katika medani mbali mbali, kuanzia ndani ya familia hadi kufikia Jimboni.

Askofu mkuu Lebulu anasema, Uinjilishaji wa kina unapania kuhakikisha kwamba, Neno la Mungu linapenya katika mifumo mbali mbali ya maisha ya waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Injili itakase na kutakatifuza medani mbali mbali za maisha kwa njia ya ushuhuda wa imani katika matendo!







All the contents on this site are copyrighted ©.