2013-12-24 09:23:50

Vipaumbele kwa sasa: ulinzi na usalama, afya na elimu pamoja na ujenzi wa Somalia mpya!


Waziri mkuu wa Somalia Bwana Abdiweli Sheikh Ahmed; amepitishwa na Bunge la Somalia kwa kishindo kwa kupata kura 243 kati ya kura 248 zilizopigwa na Wabunge, Jumapili iliyopita. Bwana Abdiweli Sheikh Ahmed anaongoza Serikali ya Somalia baada ya Wabunge kupiga kura ya maoni ya kutokuwa na imani na Waziri Abdi Farah Shirdon.

Waziri mkuu mpya Bwana Abdiweli Sheihk Ahmed ni mwanauchumi aliyebobea katika taaluma yake. Amewahi kufanya kazi katika Benki ya Maendeleo ya Kiislam iliyoko Saud Arabia. Katika hotuba yake ya shukrani kwa Bunge, Waziri mkuu amesema, Serikali yake inapania kutekeleza shughuli zake kwa kushirikiana na Bunge pamoja na taasisi nyingine na kwamba, kipaumbele cha kwanza ni: ulinzi na usalama; afya na elimu pamoja na kuanza mchakato wa ujenzi mpya wa Somalia ambayo kwa miaka mingi imeendelea kudidimia katika vita na majanga ya kitaifa!

Ni matumaini ya wapenda amani kwamba, Waziri mkuu Abdiweli Sheikh Ahmed atajielekeza zaidi katika mchakato wa kuimarisha Serikali yake ili kukabiliana na changamoto za ulinzi na usalama; haki na amani; kwani wananchi wa Somalia sasa wamechoka na vita, wanataka amani na usalama, ili kupambana na changamoto za maisha kwa utulivu zaidi.







All the contents on this site are copyrighted ©.