MERRY CHRISTMAS – HERI KWA NOELI! Kristmas ni Birthday ya mmoja katika UTATU aliyetumwa
kufanya kazi kwenye sayari hii inayoitwa dunia. Hebu tujaribu kupiga twasira. Siku
moja, huko mbinguni kulikuwa na mkutano wa Halmashauri kuu ya Utatu Mtakatifu.
Ajenda kuu
ya mkutano ilihusu kuizungumzia sayari dunia. Hasa kutokana na mabadiliko makuu yaliyokuwa
yanajitokeza hapa na pale baada ya uumbaji. Ikabidi Utatu uangalie hatima yake na
kutolea maamuzi. Uamuzi ambao ulitegemewa ubadili mfumo mzima wa maisha ya binadamu
duniani! Kwa vile ulikuwa mkutano wa kwanza toka kazi ya uumbaji ilipokamilika, ilibidi
kwanza kutathmini mwendo mzima wa uumbaji ulivyokuwa.
Mwishoni ikathibika
kwamba ni kweli “Mbingu na nchi zilishaumbwa. Awali nchi hiyo ilikuwa ukiwa, tena
utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji.” Na utatu ukakiri kwamba ulitamka
kwa pamoja, “Iwe Nuru!” (Mwa 1:30). Baada ya kuiumba Nuru “Utatu ukaiona nuru, ya
kuwa ni njema;” (Mwa 1:4). Halmashauri ikajipongeza kwa kazi hiyo nzuri na kwamba
sasa Nuru ilikuwa imeshaifukuza giza huko duniani.
“Hiyo ilikuwa Nuru halisi,
amtiaye nuru kila mtu hapa ulimwengu” (Yoh. 1:9). Nuru hiyo ni alama ya uhai, ukweli,
uwazi, haki, upendo, matumaini, furaha, uzuri, maisha bora kwa kila mkaaji wa duniani.
Lakini katika tathmini hiyo ikagundulika kwamba hali halisi ya dunia haikuwa hivyo.
Duniani kulikuwa kumetanda giza lililosababishwa na wanadamu. Watu hao walikuwa wamejitangazia
sera zao za maisha zinazoongoza kwenye mangamizo na kifo chao wenyewe binadamu.
Binadamu
walikuwa wanakandamizana, kuoneana, wanachukuana utumwa, wanatawalana ovyo, hasahasa
viongozi. Hata mwandishi mmoja wa kitabu cha Daniele katika Biblia aliandika: “Wakuu
wote wa dunia ni wanyama.” Aidha kulikuwa na umahuru uliokithiri ambao haukumtambua
tena mwumbaji wa Nuru. Wengine walidiriki hata kujiita miungu katika nafasi zao za
maisha. Mbaya zaidi watu hao walikuwa wamebobea gizani kiasi hata cha kuichukia Nuru.
Kila kitu kilikuwa kinaendeshwa gizani. Anayejaribu kuwasha walau mshumaa au koroboi
huyo anakuwa adui.
Basi baada ya mapitio hayo, mkutano ukabidi utoe maamuzi
mazito na ya haraka. Mkutano ukawa na kazi moja tu na iliyopata kauli mbiu: AZIMIO
– DUNIA. Hatimaye uamuzi uliofikiwa wa mkutano ni kuituma nafsi ya pili ya Halmashauri
kuu aende duniani. Kwa bahati nzuri nafsi hiyo ikakubali kutumwa kuja missioni kwenye
sayari hiyo pekee anayokaa binadamu. Ujio wa kijana huyo ulikuwa ni breaking nyuzzzz
kwa wakazi wa sayari dunia hasahasa kwa wanyonge. Zilikuwa ni nyuzzz kwa sababu jambo
kama hilo hawakuwahi kuliotea ndoto, kwa vile halijawahi kusikika wala kutokea popote
na halitatokea tena katika historia ya binadamu eti “Mungu azaliwe”. Aidha, hakuna
hata dini moja hapa duniani iliyowahi kuwa na ujasiri wa kutangaza AZIMIO kama hilo
la “Mungu kuwa binadamu.”
Hiyo ndiyo kufuru na ukafiri uliobobea kudai kuwa
Mungu anaweza kuzaliwa na kuwa binadamu kama binadamu wengine. Hata wayahudi wenyewe
waliokuwa wamebobea katika dini walikiita kituko hicho kuwa ni Kikwazo. Kadhalika
wataalamu wa filosofia waliowahi kutokea hapa duniani wanaothibitisha kabisa kwamba
yuko Mungu mmoja, nao pia hawakuwa na ujasiri wa kudai kwamba Mungu anaweza kuwa binadamu,
akae pamoja na binadamu na kushirikiana na binadamu. Fikra hiyo haiingii kichwani
na ni kitendo cha kumdhalilisha Mungu. Kwamba haiwezekani kitu kilicho kikamilifu
kabisa kama Mungu kichukue hali ya ukiumbe, kiwe na mwili ulio na mipaka na udhaifu.
Wagiriki walio magwiji wa filosofia kitendo hicho walikiita ni Upuuzi.
Kwa
upande wa Halmashauri Kuu, Utatu ulitegemea Nuru hiyo ingepokewa kwa kishindo hasa
na watu waliobobea katika imani kwa Mungu mmoja, na wale wataalamu wa filosofia kwa
vile wanaupana wa kuelewa mambo. Kumbe ikawa kinyume “Alikuja kwake, wala walio wake
hawakumpokea” (Yoh. 1:11). Mtazamo huo hasi na wa ukosoaji wa ujio wa nafsi hiyo ya
pili duniani, umedumu miaka elfu mbili na unaendelea. Mbaya zaidi ikaja kugundulika
kwamba AZIMIO – DUNIA likaundiwa vyama vingi vya upinzani hapa duniani. Hata hivyo,
utekelezaji wa AZIMIO ulipofika, Nafsi hiyo ya pili akazaliwa kwa sababu: “macho ya
chura hayawezi kumzuia ng’ombe kunywa maji.” Kuthibitisha hilo unaona hata mpangilio
wa nyakati hapa duniani umepangwa kutokana na ujio wake Yeye.
Kila tunapotamka
mwaka katika historia tunasema Kabla au Baada ya kuzaliwa Kristu. Swali linalowakanganya
baadhi ya wakazi na wataalamu wa dunia juu ya Mungu kuwa binadamu, linapata jibu kutokana
na msemo mmoja wa kilatini wa Mababa wa Kanisa unaoanisha hilo: "Quod erat permansit;
quod non erat assumpsit," yaani, “Kile kilichobaki kama kilivyokuwa hata baada ya
kujiunga na kile ambacho hakikuwepo.” Mungu kwa kuchukua Mwili na kuzaliwa, anabaki
kuwa kama alivyokuwa kabla yake. Anabaki kuwa Mungu na sifa zake zote za kimungu:
yaani anabaki kuwa Mungu mmoja, wa Milele, Mwenyezi, asiye na mwanzo wala mwisho,
yupo pahala pote, habadiliki, ni mkuu daima nk. Alikuwa ni kila kitu, alijua kila
kitu, aliweza kila kitu, na aliishi katika heri pamoja na Baba. Kabla hakuwa binadamu,
hakuwa dhaifu, hakuwa mdhambi. Anabaki kuwa hivyo hata baada ya kuwa binadamu.
Huyo
ni NURU ya kweli ikashuka duniani kulikokuwa na giza, ikabaki kuwa NURU ili ilishinde
hilo giza la dunia hii. NURU hiyo haijawahi kamwe kutokea na wala haitatokea kamwe
kwa sayari nyingine za ulimwenguni zilizowahi kugundulika. Kumbe daima itabaki sayari
dunia kuwa makao ya NURU. Kwa hiyo kizazi cha binadamu hakitaweza tena kujidai kuwa
kama Mungu kama ilivyowahi kutokea kwa baadhi ya wafalme, wakuu na watawala kujifanya
miungu na kuwataka wengine wawatumikie. Hilo kamwe halitatokea tena kwa sababu tayari
Mungu mwenyewe ametuondolea uvivu kwa Yeye mwenyewe kujifanya binadamu na kuwa sawa
kama sisi.
Kazi kuu ya Nuru iliyofika duniani ni kupambana na giza. Huo ni
mvutano na patashika ya kudumu: “Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa
nuru ya watu. Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza” (Yohane 1:4-5), yaani
mapambano kati ya Nuru itokayo mbinguni na giza lililoshamiri ulimwenguni linalojiona
liko katika kusambaratishwa, hivi linatafuta daima jinsi ya kuizima hiyo nuru. Mwanga
au nuru hiyo ni Nyota, ambaye Majusi waliongozwa nayo toka Mashariki ya mbali. Ni
Nuru inayowavuruga wale ambao walikuwa wanajisikia vizuri sana kufanya shughuli zao
gizani. Wale waovu, wanaopenda zaidi giza kwani nuru inawaumbua na kunawaletea maudhi.
Kuna binadamu wengine walikuwa wanajidhania kuwa wao ndiyo nuru au myanga
badala ya kuutangaza na kuutolea ushuhuda NURU halisi. Tuige mfano wa Yohane Mbatizaji
aliyesema kuwa yeye ni mshuhuda tu siyo nuru, bali itafika Nuru yenyewe ambaye ni
Yesu wa Nazareti. Nasi tuwe mashahidi wa Nuru na siyo kujifanya Nuru. Hiyo ndiyo Christmas!
Licha
ya kushuhudia Nuru, pia tuongozwe nayo, kama unavyotuhimiza utenzi wa Zakari, “Kwa
njia ya rehema za Mungu wetu, ambazo kwa hizo mwangaza utokao juu umetufikia, kuwaangaza
wakaao katika giza na uvuli wa mauti, na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani.”
(Luka 1:78-79). Tunahitaji kuongozwa na Nuru katika giza hili la maovu, la mapambano,
la kukosa amani, na la vita. Hiyo ndiyo Noeli!
Nuru hii walianza kuiona Wachungaji
waliokuwa wanachunga kondoo usiku gizani. Wachungaji hao wanawawakilisha wanyonge
wote, maskini wote, walio katika giza la masumbuko. Watu kama hao waongozwe na Nuru.
Hiyo ndiyo Christmas!
Tusifurahie kukaa gizani, bali tufurahi kufikiwa na Nuru,
kama alivyofurahi mzee Simeon pale alipomshika huyo mtoto mikononi na kusema: “Kwa
kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, uliouweka tayari machoni pa watu wote. Nuru
ya kuwa mwangaza wa mataifa na kuwa utukufu wa watu wako Israeli.” (Luka 1:30-32).
Ama kweli yatubidi tufurahi sisi tulio katika giza la mauti na la mateso ya kila aina.
Lakini tumeona Nuru kama asemavyo Mateo pale Nuru hiyo ilipoanza kuhubiri: “Watu wale
waliokaa katika giza wameona mwanga mkuu, nao waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti
mwanga umewazukia.” (Mt 4:15-16).
Ndugu zangu, Ulimwengu wa leo umeshehena
giza la mambo mengi. Kadhalika kuna wengi wanajitokeza kujifanya Nuru kutusaidia kuchagua
iwe kiuchumi, kisiasa, kidini, nk. Hadi hujui tena ipi ni nuru ya kweli. Katika safari
yetu hapa bondeni kwenye machoni, sisi tuangazwe na kuongozwa na Nuru ya kweli iliyoshuka
toka mbinguni. Hii ndiyo faida kubwa ya kusherekea Kristmas kwa mkristu. Yaani kule
kubahatika kujua kwamba Nuru imetwaa mwili, na kukaa kwetu, na ni Nuru inayoniangaza
katika njia ya ulimwengu huu uliotanda giza. Yesu ndiye ni Nuru ya ulimwengu. Ukiipokea
Nuru hiyo, na kushika sera zake, hapo utakuwa umelienzi AZIMIO-DUNIA la Utatu Mtakatifu.
Utakuwa umeelewa maana yake nini kusherekea Noeli. Ndipo kweli utastahili kuimba na
hata kuimbiwa pamoja na Nuru: MERRY CHRISTMAS na HERI KWA NOELI. Tumshukuru na
Tumsifu Yesu Kristu. Milele Amina. Padre Alcuin Nyirenda OSB Sant’Anselmo-Roma.