Tafakari ya Neno la Mungu, Siku kuu ya Noeli, 2013
Mpendwa mwanatafakari, unayeitegea sikio Radio Vatican, kwanza ninakutakieni heri
na baraka tele za kuzaliwa Mwana wa Mungu. Leo ni Krismas,
ni Noeli, ni neema ya Mungu iliyofunuliwa kwa ulimwengu mzima. Kwa hakika ile ahadi
ya Mungu aliyoitoa tangu zamani sasa imefunuliwa na hivi tunafurahi na kushangilia
tukiimba utukufu kwa Mungu juu na amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema. Mtoto
Emanueli aliye na uweza wa kifalme mabegani mwake, Mungu pamoja nasi amezaliwa kwa
ajili yetu. Kanisa duniani kote linaimba “pangoni Batlehemu amezaliwa Mtoto Yesu,
twendeni sote tukamwone na kumpa zawadi”
Nabii Isaya anayeishi karne ya nane
kabla ya Kristu, anaonesha katika masomo ya sherehe za Noeli jinsi Waisraeli wanavyofurahi
kurudi nyumbani toka utumwani Babeli. Wanafurahi kwa sababu wamekaa chini ya kandamizo
la utumwa kwa muda mrefu, na kandamizo hilo lilikuja kwa sababu wao wenyewe walishindwa
kutii mausia ya Mungu wakaingia katika ugomvi kati yao na hivi wakapelekwa utumwani.
Sasa Nabii Isaya akiona mwisho wa utumwa huo katika maono anaimba akisema “watu wote
waliokwenda katika giza wameiona nuru kuu na wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa
mauti nuru imewaangaza”
Uaguzi huu wa Nabii Isaya unakamilika kwa kuzaliwa
Masiha, Mwana wa Mungu, aliye mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele
na mfalme wa amani. Enzi yake haina mwisho, atahukumu kwa haki. Na kwa hakika hakuna
mfalme mwingine kabla na baada yake aliyeweza kuwa na sifa hizi.
Katika nyakati
zetu hisi yawezekana nasi tukawa tuko utumwani, tuko katika taabu mbalimbali kama
vile ukosefu wa mahali pazuri pa kuishi, shida ya umeme, maji, sukari, rushwa na ugomvi
kati yetu, maudhulumu na mauaji ya watu, pamoja na ajali barabarani. Je haya amesababisha
nani? Ni sisi wenyewe. Sasa leo Nuru imetushukia kutoka mbinguni kama tulivyokuwa
tukiimba wakati wa majilio “ushukie Masiha kuwakoa watumwao” Je, kuzaliwa kwa Bwana
au kushuka kwa Nuru hii kwatufanya kweli tuonje lile pendo la kweli walilolionja Waisraeli
toka utumwani Babeli? Ewe mpendwa, Mwana wa Mungu ni Emanueli anakuja kutuondolea
utumwa wa shetani cha msingi tuaanze pamoja naye kuacha ubaya na kutenda wema.
Kuacha
ubaya na kutenda wema ni ujumbe kamambe ambao Mtume Paulo anamtumia Mtakatifu Tito
akimsistizia kuwa Neema ya Mungu Mwokozi inayookoa wanadamu wote imefunuliwa kwetu
na hivi kazi yetu kama twataka kuifaidi neema hiyo ni kuambatana na maisha ya uongofu,
maisha ya kupokea na kuzitumia neema za Mungu pamoja nasi yaani Emanueli. Kuzaliwa
kwa Kristu ni amani na uhuru kwa wana wa Mungu. Kuzaliwa kwa Kristu ni ufunuo mkamilifu
wa Mungu kwetu kwa maana tangu zamani Mungu alisema nasi kwa njia ya mababu, manabii
na sasa anasema nasi kwa njia ya Masiha, Mwanae mpenzi tunayepaswa kumfuata.
Mpendwa
mwana Noeli, Mwinjili Luka akitupeni habari ya furaha, kwanza anamweka Bwana katika
mazingira ya mwanadamu. Anaweka mbele yetu kwanza jambo la kijiografia na la kihistoria,
akisimulia juu ya Masiha anayezaliwa wakati wa mfalme wa Kirumi Kaisari Augusto, pia
anazaliwa Betlehem kijiji cha wachungaji kama ilivyokuwa imeaguliwa kwamba atazaliwa
katika ukoo wa Daudi. Hili laonesha kuwa Masiha anaingia katika maisha ya mwandamu.
Pamoja na hilo pale pangoni Betlehemu anashuhudiwa na wachungaji kielelezo cha upendo
wa Mungu kwa wote na hasa walio fukara na maskini, na kwa jinsi hiyo Mungu atufundisha
kushinda uovu si kwa vita bali kwa upendo na msamaha.
Wote twatambua kuwa
wachungaji wakati ule walikuwa ni watu wa kulala machungani, waliodharauliwa na hata
hawakuruhusiwa kuingia kwenye masinagogi, walikuwa wakisadikika kuwa waongo na wagomvi.
Mwana wa Mungu anaona hao ndio wapewe habari ya kuzaliwa kwake wakiwa wa kwanza. Maana
yake Mungu ni kwa ajili yao na anachagua kukaa katikati yao yaani walio maskini. Mwinjili
Yohane anaweka mbele ya mataifa Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili na akakaa kwetu.
Masiha ni Neno wa Mungu ambaye anatumwa na Mungu kwetu kwa sababu ya upendo upeo.
Ni nuru ileile ambayo Nabii Isaya anaitanganza katika Agano la kale ya kwamba miisho
yote ya dunia imeiona nuru na wokovu wa Mungu.
Mungu amefanyika mwili nasi
tukauona wokovu wake na hivi tunaalikwa kusikiliza na kutenda kadiri ya mapenzi yake.
Mwinjili Yohane anatupatia fumbo la umwilisho kielelezo wazi cha upendo wa Mungu,
Mungu anayejishusha na kutwaa mwili wako dhaifu! Anataka kugeuza mwili wako uwe mwili
wa utukufu. Kwa fumbo hili la Bwana kukaa kwetu ni fundisho la amani kwa mataifa,
kumbe kugombana tishio dhidi ya upendo katika jamii uliowekwa kwa njia ya fumbo la
umwilisho. Yafaa kufikiri kidogo juu ya vita vinavyoendelea duniani.
Kumbe
Neno akafanyika mwili ni nuru na amani kwa watu wote. Ni sura na utukufu wa Mungu
Baba na kielelezo cha mapendo yasiyopimika kwa Mwanadamu. Ni mwaliko kuombea amani
duniani kote na hasa katika mataifa yaliyo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, mfano
huko Siria.
Ninakukumbusha kuwa Bwana amekuja na kukaa kwetu, maana yake anakaa
kwenye familia kumbe ni sherehe ya familia ni siku za kukaa pamoja Baba mama na watoto.
Na kama vile ambavyo mtoto anapozaliwa tunapeleka habari ya furaha kwa majirani basi
kukaa kwetu pamoja na Bwana katika familia kuwe ni chimbuko la habari njema ya furaha
kama Wachungaji walivyopeleka habari njema ya furaha kwa watu wote.
Kumbuka
kule Betlehemu Bwana alikosa nafasi katika nyumba ya wageni na hivi asije akakosa
nafasi katika moyo wako katika sherehe hizi za Noel na daima. Nafasi ya Bwana yapaswa
kutayarishwa daima kwa maisha ya sala na sakramenti. Kuna desturi ya kubatiza watoto
katika sikukuu ya Noeli, yafaa kuelewa kuwa ni nafasi muhimu na ya pekee inayotayarisha
mahali Bwana atakapokaa katika mtoto huyo, kumbe wazazi itunzeni nafasi iletwayo kwetu
kwa njia ya ubatizo. Ninakutakieni heri na baraka tele za Mungu leo na daima. Tumsifu
Yesu Kristo na Bikira Maria. Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya,
C.PP.S.