Dumisheni Injili ya Uhai dhidi ya Utamaduni wa kifo!
Noeli ni Siku kuu inayotoa nafasi kwa waamini kufanya tafakari ya kina kuhusu Fumbo
la Umwilisho, Neno wa Mungu alipofanyika mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu, kwake Yeye
Bikira Maria akawa mwanadamu, katika mambo yote akawa sawa na binadamu isipokuwa hakutenda
dhambi!
Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha
kwamba, wanalimwilisha Fumbo hili katika vipaumbele na uhalisia wa maisha yao. Noeli
kiwe ni kipindi cha upendo na mshikamano wa dhati kati ya watu; haki na amani kati
ya mataifa! Noeli ni nafasi kwa waamini kuonja ule mshikamano wa upendo na ugudu kutoka
kwa Kristo, ili kumkomboa mwanadamu aliyekuwa anatembea katika lindi la dhambi na
uvuli wa mauti. Waamini wanakumbushwa kwamba, Mungu ni upendo, kumbe Noeli ni Siku
kuu ya Imani, Matumaini na Mapendo.
Askofu msaidizi Eusebius Nzigilwa wa Jimbo
kuu la Dar es Salaam, Tanzania akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam,
ili kutoa salam na matasgi mema kwa Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 2013, anawaalika waamini
kubadilika kwa kuthamini na kushuhudia Injili ya Uhai, dhidi ya utamaduni wa kifo,
unaokumbatia kwa namna ya pekee sera na vitendo vya utoaji mimba! Haya ni mambo ambayo
yanaanza kuonekana kuwa ni kawaida, lakini ukweli ni kwamba, Jamii inakwenda kinyume
cha ukweli wa Injili ya Uhai.
Waamini na watu wenye mapenzi mema wanaalikwa
kusimama kidete kulinda na kutetea uhai ambayio ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi
Mungu. Waamini wajitahidi kuyafahamu Mafundisho Jamii ya Kanisa kuhusu maisha ya ndoa
na familia pamoja na changamoto zake, ili wasimezwe na malimwengu kwa kukumbatia sera
za utoaji mimba!
Sherehe za Noeli si kipindi cha kujirusha! Kufanya maasi kwa
kutojiheshimu wala kuzingatia maadili na utu wema! Askofu msaidizi Eusebius Nzigilwa
anasema kwamba, inasikitisha kuona kwamba, wakati wa Siku kuu kama Noeli, vitendo
vya uvunjifu wa sheria, amani na maadili vinaongezeka kwa wingi. Hapana, huu ni mwelekeo
potofu, Noeli kiwe ni kipindi cha kujitakatifuza kwa njia ya Sakramenti za Kanisa,
Neno la Mungu na matendo ya huruma, kielelezo makini cha imani tendaji! Waamini wajitahidi
kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao adili na manyofu!
Askofu
msaidizi Eusebius Nzigilwa anazipongeza taasisi na wale wote wanaosimama kidete kulinda
na kutetea Injili ya Uhai. Anawataka waendelee kusonga mbele kwa ari na mwamko mkubwa
zaidi bila ya kuogopa wala kuogopeshwa na wale wanaotaka kukumbatia utamaduni wa kifo!
Jamii inapaswa kutambua na kuthamini zaidi uhai na kwamba, maisha ya binadamu si jambo
la kuchezea!
Askofu msaidizi Nzigilwa amevishukuru na kuvipongeza vyombo vya
hanari nchini Tanzania kwa kazi nzuri vinavyofanya kwa ajili ya ustawi na maendeleo
ya watanzania wengi. Amevitaka vyombo hivi kuzingatia: taaluma na maadili ya kaz;
weledi na utu wema. Vyombo vya habari visikubali kutumiwa na wajanja wachache kwa
ajili ya kupandikiza mbegu ya utamaduni wa kifo kwani hili linaweza kuwa ni janga
la kitaifa kwa siku za usoni kama inavyojionesha kwa baadhi ya mataifa ambayo yalikumbatia
utamaduni huu na kwa sasa yanajuta kufanya hivyo!
Noeli iwe ni Siku kuu ya
Familia na Mshikamano wa Upendo kwa majirani! Watu wajifunze kuonesha na kuonjeshana
ukarimu kwani jambo hili ni sehemu ya vinasaba vya tamaduni nyingi za Kiafrika!