2013-12-23 08:24:41

Ujumbe wa Noeli kwa Mwaka 2013 kutoka kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni


Simulizi la kuzaliwa kwa Mtoto Yesu katika Agano Jipya linaonesha jinsi ambavyo Mtoto Yesu alizaliwa katika mazingira ya kawaida kabisa, akizungukwa na wachungaji waliokuwa wanachunga mifugo yao kondeni. Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali, hali wakiongozwa na nyota walikuwa wanamtafuta Mfalme wa Wayahudi. RealAudioMP3

Watu wote hawa walikuwa katika safari ya kutafuta matumaini mapya kwa ajili ya ulimwengu. Usiku ni kipindi cha kufanya tafakari ya kina kuhusu matukio mbali mbali yaliyopita, ili kuwa tayari kujiandaa kwa ajili ya kukabiliana na yale yatakayojiri katika siku mpya.

Mwinjili Yohane anaanza simulizi la kuzaliwa kwa Mtoto Yesu kwa kusema kwamba, hapo mwanzo kulikuwepo Neno, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Huyu ndiye Neno wa Mwanga na maisha ya uzima wa milele, anayekuja ulimwenguni kufukuza giza linaloendelea kumwelemea mwanadamu. Mwinjili Luka kwa upande wake anasema kwamba, nikwa njia ya rehema za Mwenyezi Mungu, ambazo kwa hizo mwangaza utokao juu umewafikia watu wake, ili kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli wa mauti. Kwa hakika Neno la Mungu ni taa ya kuangazia njia ya waja wake.

Huu ndio ujumbe wa Noeli kwa Mwaka 2013 kutoka kwa Dr. Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Anasema, binadamu ambaye kimsingi ni mavumbi anahitaji kuongozwa na Mwenyezi Mungu, ili kugundua njia ya haki, amani, upatanisho na utimilifu wa maisha. Mwanadamu anahitaji mwanga wa Neno la Mungu ili kumwongoza katika njia za Kimungu sanjari na kuendelea kumlilia Mungu wa maisha aweze kuwaongoza katika haki na amani kwa kutambua kwamba, hapa duniani binadamu ni msafiri na wala hana makazi ya kudumu.

Dr. Tveit anasema wakati wa Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa kumi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, wajumbe walifanya hija kwa sala za pamoja, warsha na mikutano, wakasafiri katika viunga vya Jamhuri ya Watu wa Korea na kinzani zake. Wametambua kwamba haki na amani inaweza kupatikana ikiwa wananchi wa Korea zote mbili wataondokana na uhasama unaoendelea kuwagawa katika: utaifa, makundi ya watu na familia.

Kama wajumbe wa mkutano mkuu wameguswa na mahangaiko ya wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum huko Mashariki ya Kati na Eneo la Maziwa makuu, lakini kwa namna ya pekee sana, nchini DRC. Wajumbe wamelaani sera za baadhi ya viongozi wa Serikali kutumia udini kama njia ya kuhalalisha matumizi ya nguvu dhidi ya baadhi ya watu ndani ya Jamii.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujiunga pamoja nao katika hija ya kutafuta amani ya kweli duniani. Wanapenda kufanya hija ya pamoja kwa kuonesha umoja na mapendo kati yao. Wanaongozwa na Mfalme wa Amani kutafuta amani hata katika sehemu ambazo si muafaka. Hivi ndivyo Dr. Olav Fyske Tveit, anavyohitimisha salam na matashi mema ya Noeli kwa Mwaka 2013 kutoka kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni.








All the contents on this site are copyrighted ©.