Mahujaji 55 kutoka Tanzania wameanza hija ya kiroho Nchi Takatifu
Changamoto katika kukoleza imani tendaji: “Simameni imara katika imani” (1Kor 16:13).
Hii ndiyo dira na mwaliko wa Kanisa kwa nyakati zote, na zaidi sana katika wakati
wetu huu wa kihistoria ambapo kumejitokeza sana kuyumba kwa imani miongoni mwa waamini
na hivi kuamsha uhitaji wa Uinjilishaji Mpya na wa kina kwa matendo. Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani lilipenda kuwashirikisha
waamini tafakari ya kina kuhusu Imani ili iwaongoze wana familia ya Mungu ”katika
kuishi kiaminifu imani ile tunayoishiriki pamoja, imani ambayo baada ya kuipokea tunapaswa
kuilinda, kuitunza na kuikuza. Tunataka mtambue siku zote kuwa sisi, kwa wajibu tuliopewa
na Kanisa, tunapaswa kufundisha, kuilinda na kuifanya imani yenu ikue, na wala “si
kwamba tunatawala imani yenu; bali tu wasaidizi wa furaha yenu; maana kwa imani yenu
mnasimama” (2Kor 1:24). Ni sala yetu kuwa, katika Mwaka huu wa Imani, tutafanya
bidii ya makusudi kuijua, kuiishi na kuwashirikisha wengine imani yetu, ili “sote
tuufikie umoja wa imani na kumjua Mwana wa Mungu; tuwe watu waliokomaa na kuufikia
utimilifu wake Kristo mwenyewe” (Efe 4:13). Baada ya Maadhimisho ya Mwaka wa
Imani nchini Tanzania, kundi la mahujaji 55 kutoka Tanzania limeondoka Jijini Dar
es Salaam, Jumapili tarehe 22 Desemba 2013 kuelekea Nchi Takatifu na Misri, ili kukoleza
imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, tayari: kuikiri, kuiadhimisha katika Liturujia
na Sakramenti za Kanisa; kwa kuimwilisha katika maisha adili yanayoongozwa kimsingi
na Amri za Mungu pamoja na kuimwilisha katika Sala, kielelezo cha imani tendaji! Mahujaji
kutoka Tanzania wanatembelea maeneo ya historia ya ukombozi kadiri ya Maandiko Matakatifu:
Wanatembelea eneo alilozaliwa Yesu; mahali alipoteswa, akafa na kufufuka. Kipindi
hiki kuanzia tarehe 23 Desemba hadi tarehe 31 Desemba 2013, utakuwa ni muda wa sala
na tafakari ya Neno la Mungu. Kundi la mahujaji kutoka Tanzania linaongozwa na Padre
Desiderius Rugemalira, Paroko wa Parokia ya Kilimahewa, Jimbo kuu la Dar es Salaam.
Linawajumuisha Mapadre 5, Watawa 7 na wengine wote waliobaki ni Waamini walei kutoka
Majimbo mbali mbali ya Kanisa Katoliki nchini Tanzania.